DKT. MADALLA AWATAKA WADAU KUTUMIA FURSA ZA UVUVI ILI KUONGEZA UZALISHAJI, AJIRA NA KIPATO
Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbemaji Nchini, Dkt. Nazael Madalla amewataka wadau wa sekta ya uvuvi nchini kutumia ipasavyo fursa zilizopo katika sekta hiyo kwa kuwekeza katika shughuli mbalimbali za uvuvi ili kuongeza uzalishaji, kukuza ajira na kuinua kipato cha wananchi.
Akizungumza kuhusu maendeleo ya sekta ya uvuvi kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi leo Novemba 21, 2026 Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya mvuvi Duniani, Dkt. Madalla amesema sekta hiyo ina fursa nyingi za kiuchumi ambazo zikitumika vizuri zinaweza kuwa chachu ya maendeleo kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
"Uwekezaji katika shughuli za uvuvi, ufugaji wa samaki, uchakataji na biashara ya mazao ya uvuvi ni miongoni mwa maeneo yanayoweza kutoa ajira kwa vijana na wanawake, kwani yanaongeza thamani ya mazao hayo na kupanua masoko" amesema Dkt. Madalla
Aidha, Dkt. Madalla amesisitiza umuhimu wa wadau kutumia teknolojia na vifaa vya kisasa katika shughuli za uvuvi ili kuongeza tija, kupunguza upotevu wa mazao na kuhakikisha rasilimali za uvuvi zinatumika kwa kuzingatia misingi ya uvuvi endelevu.
Vilevile, Dkt. Madalla amesema ushirikiano baina ya Serikali na sekta binafsi ni muhimu katika kufanikisha maendeleo ya sekta hiyo, akiwataka wadau kuchangamkia fursa zilizopo ili kuongeza uzalishaji, ajira na kipato, sambamba na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Pwani, ambaye ni Afisa Uvuvi, Bw. Kenneth Mrope amesema maendeleo ya Sekta ya uvuvi hayawezi kuwa endelevu kama hakuna usimamizi madhubuti wa rasilimali ya uvuvi, hivyo ni vyema wavuvi na wadau wote kuzingatia Sheria, kanuni na taratibu za uvuvi na kuachana na uvuvi haramu.