Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

DKT. BASHIRU AKAGUA SHAMBA LA MIFUGO NGERENGERE, ATOA MAAGIZO MAGEUZI SEKTA YA MIFUGO

Imewekwa: 23 November, 2026
DKT. BASHIRU AKAGUA SHAMBA LA MIFUGO NGERENGERE, ATOA MAAGIZO MAGEUZI SEKTA YA MIFUGO

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa leo Novemba 21, 2026 ametembelea na kukagua shughuli za uzalishaji zinazofanyika katika Shamba la Uzalishaji wa Mifugo la Ngerengere Mkoani Morogoro, ambapo pia amefanya mazungumzo na watumishi wa shamba hilo ikiwa ni pamoja na kupata maoni yao juu ya uendeshaji wa mashamba ya mifugo yaliyochini ya wizara.

Ziara hiyo ni mwendelezo wake wa kukagua mashamba ya mifugo ya serikali  ambapo hadi sasa ameshatembelea Shamba la Mifugo Kitulo lililopo mkoani Njombe, Shamba la Sao Hill la Iringa, Mabuki la Mkoani Mwanza na sasa Shamba la Ngerengere mkoani Morogoro ambayo uzalishaji wa mashamba hayo unatarajiwa kuboresha ufugaji nchini kupitia upatikanaji wa mitamba na mbegu bora za mifugo ili kuongeza tija kwa wafugaji kwa kufanya ufugaji wa kisasa.

Akizungumza na watumishi wa shamba la Ngerengere Mhe. Dkt. Bashiru alitoa fursa ya majadiliano ya wazi kuhusu maoni na mapendekezo ya namna ya kuendesha mashamba ya mifugo ya serikali ili kuwa na usimamizi wenye ufanisi na tija utakaoongeza uzalishaji na kukidhi mahitaji ya wafugaji nchini.

Majadiliano hayo, yalijikita katika kupendekeza taasisi iliyochini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi itakayoweza kusimamia na kuyaendesha mashamba hayo, ambapo Mhe. Waziri Dkt. Bashiru aliagiza kuandaliwa kwa andiko lenye mapendekezo ya kitaalam kuhusu namna ya kuyaendesha mashamba hayo, ambapo katika maoni na mapendekezo ya awali katika majadiliano baina ya Waziri na Watumishi wa Shamba la Ngerengere, Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) ilipendekezwa, kuwa taasisi inayoweza kuyasimamia mashamba hayo na kuwa na tija.

Kwa Upande wake, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Dkt. Fabian Madele alisema kuwa miongoni mwa mipango iliyowekwa na wizara katika mwaka huu wa fedha ni kuboresha mbari kwa ajili ya mitamba ya ng'ombe wa maziwa katika mashamba ya uzalishaji mifugo ya serikali ikiwemo LMU Ngerengere kupitia Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabia Nchini (C-SDTP).

Hata hivyo, Shamba hilo linakabiliwa na Changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa maji ya uhakika kwa ajili ya  mifugo na uwepo wa baadhi ya magonjwa ya mifugo kama vile ugonjwa  wa miguu na midomo(FMD), ugonjwa wa Kupe  ambapo Waziri aliagiza mpango wa dharura wa kutoa chanjo kwa mifugo huku changamoto ya maji ikihitaji ushirikiano na taasisi zingine za kisekta ikiwemo wizara ya maji ambapo tayari mazungumzo yameshaanza ili kupata kisima cha maji cha uhakika.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo