Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

DKT. MADELE AITAKA NARCO KUONGEZA UBUNIFU WA UZALISHAJI KIBIASHARA.

Imewekwa: 27 May, 2026
DKT. MADELE AITAKA NARCO KUONGEZA UBUNIFU WA UZALISHAJI KIBIASHARA.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Sekta ya Mifugo, Dkt. Fabian Madele, ameiagiza Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kuongeza ubunifu katika utekelezaji wa majukumu yake ya kibiashara ili kuimarisha mchango wa sekta ya mifugo katika uchumi wa nchi.

Dkt. Madele ametoa agizo hilo leo Mei 19, 2026 alipofanya ziara katika Ranchi ya Mzeri Hill iliyopo katika Wilaya za Handeni na Korogwe mkoani Tanga kwa lengo la kukagua shughuli za uzalishaji na maendeleo ya ranchi hiyo.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kusisitiza matumizi ya sayansi na teknolojia katika sekta ya mifugo ili kuyafikia matarajio ya wafugaji pamoja na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya Taifa.

Aidha, ameitaka NARCO kuongeza uzalishaji wa malisho ya mifugo ili kuhakikisha upatikanaji wa malisho bora na ya kutosha kwa mifugo katika nyakati zote za mwaka, hatua ambayo itasaidia kuongeza uzalishaji wenye tija na kuhimili changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Dkt. Madele pia amesisitiza umuhimu wa ushirikiano na mshikamano miongoni mwa watumishi wa kampuni hiyo ili kuwezesha utekelezaji bora wa majukumu ya msingi ya NARCO ambayo ni kuzalisha, kuendeleza na kufanya biashara ya mifugo pamoja na kusimamia ranchi za Taifa kwa tija ya kiuchumi.

Akizungumza kuhusu mikakati ya ranchi hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa NARCO Bw. Mohamed Mbwana, amesema ranchi hiyo imejipanga kuongeza uzalishaji wa malisho kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji endelevu wa chakula cha mifugo na kuboresha uzalishaji.

Kwa upande wake, Meneja wa Ranchi ya Mzeri Hill Bw. Greyson Mutabazi, amesema ranchi hiyo ina jumla ya hekta 49.7 zilizogawanywa kwa matumizi mbalimbali ya uzalishaji na uwekezaji, ambapo hekta 41.9 zimetengwa kwa ajili ya vitalu vya uwekezaji.

“Mgawanyo huo umewezesha matumizi bora ya ardhi kwa shughuli za ranchi pamoja na uwekezaji mbalimbali unaofanyika ndani ya ranchi,” amesema Mutabazi.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo