DKT. BASHIRU AIPONGEZA INADES MAADHIMISHO YA SIKU YA PUNDA
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amelipongeza shirika lisilo la Serikali la “INADES” kwa kufanikisha maadhimisho ya kitaifa ya Punda yaliyofanyika Mei 08,2026 mkoani Geita.
Balozi Dkt. Bashiru ametoa pongezi hizo Mei 20,2026 mara baada ya kutembelewa ofisini kwake na Mkurugenzi wa shirika hilo Bi. Jacqueline Nicodemus ambaye alifika kwa kwa lengo la kuwasilisha fupi ya utekelezaji wa maadhimisho hayo.
“Yapo makundi ya watu yanajifunika kwenye blanketi la kuwahudumia wananchi ila baada ya muda unakuta wapo kwenye mgongano wa kimaslahi baina yao na Serikali hivyo tunapopata wadau mnaotusaidia kweli tunafarijika sana” ameongeza Balozi Dkt. Bashiru.
Aidha Balozi Dkt. Bashiru amelitaka shirika hilo kwa kushirikiana na ofisi yake kutafsiri mwongozo wa ustawi wa mnyama huyo kwa lugha ya kiswahili ili iwe rahisi kueleweka na watu wengi zaidi tofauti na ilivyo hivi sasa ambapo mwongozo huo umeandaliwa kwa lugha ya kiingereza pekee.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa shirika hilo Bi Jacqueline Nicodemus mbali na kuishukuru Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa ushirikiano waliotoa katika kufanikisha maadhimisho hayo ameainisha mafanikio waliyopata kupitia tukio hilo kuwa ni pamoja na kufikisha elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa mnyama punda, kutoa huduma za matibabu kwa wanyama hao na kutoa hamasa kwa jamii ya mkoa wa Geita na Taifa kwa ujumla kuendelea kulinda ustawi wa mnyama huyo.