WAZIRI NDAKI, AIPONGEZA BODI YA (MPRU) KWA KAZI NZURI.

Imewekwa: Wednesday 26, May 2021

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb), amewapongeza wajumbe wa bodi ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU) kwa kazi nzuri wanayoifanya licha ya changamoto wanayopitia kwenye maeneo ya hifadhi za bahari inayosababishwa na uvamizi wa shughuliza uvuvi.

Waziri Ndaki amesema hayo leo (12.05.2021) katika ofisi ndogo za wizara hiyo zilizopo katika jengo la Benki ya NBC, jijini Dodoma alipokuwa kwenye kikao na wajumbe wa bodi hiyo ili kufahamu kazi zilizotekelezwa na bodi hadi sasa.

Mhe. Ndaki amesema amepitia maeneo mengi ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu katika mikoa ya Tanga, Pwani katika Kisiwa cha Mafia, Mtwara na Dar es salam, ambapo ameona kazi nzuri ambayo bodi inatekeleza yenyewe na ni moja ya taasisi inayofanya vizuri katika kuhakikisha uhifadhi wa Bahari ya Hindi unakuwa salama.

Aidha, amesema licha ya kazi nzuri MPRU inakabiliwa na changamoto ya wavuvi wanaovamia na kuingia kwenye maeneo tengefu na kusababisha uharibifu wa maeneo hayo, kwa hiyo wizara ina kazi ya kuhakikisha inaelimisha jamii ya wavuvi kufanya shughuli za uvuvi kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.

Pia, amesema MPRU inasaidia kuongeza uchumi wa nchi pamoja na kuhifadhi na kulinda maeneo ya utalii na kuongeza watalii kuingia kwa wingi nchini.

Waziri Ndaki amebainisha kuwa changamoto zinazoikabili taasisi hiyo, wizara inazichukua na kuangalia namna ya kuzitatua kupitia bajeti ijayo ya mwaka wa fedha 2021/22, ambayo inatarajiwa kusomwa bungenihivi karibuni.

Naye, mwenyekiti wa bodi ya wadhamini ya Uhifadhi wa Bahari na Maeneo Tengefu, Dkt. Bonaventura Baya,amemshukuru Waziri Ndaki kwa kukubali kukaa na bodi hiyo nakusikiliza mawasilisho yao ya kazi ambazo wamezifanya na kuzitekeleza tangu alipoapishwa kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi.

.