Waziri Mpina akabidhiwa madawa ya kuogeshea Mifugo katika zoezi la uogeshaji Mifugo -CHATO

Imewekwa: Monday 17, December 2018

Katika kipindi hiki cha Serikali ya awamu ya Tano,mimi nikiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, nitaboresha huduma za Mifugo ili tupate Mazao ya Mifugo yaliyo Bora ikiwa ni pamoja na kuogesha Ng'ombe wetu mara kwa mara ili kuua wadudu waenezao Magojwa kwa Mifugo.

Hayo yamesemwa Leo na Mhe.Luhaga Joelson Mpina,Waziri wa Mifugo na Uvuvi alipokuwa akizindua kampeni ya Kitaifa ya Uogeshaji Mifugo Katika Halmashauri ya Wilaya ya Chato kata ya Buzilayombo Mkoani Geita.

Mpina amesema kuwa Tanzania inajumla ya Majosho 2,428 kati ya hayo Majosho 1,018 hayafanyi kazi,amewashauri wafugaji kuunda ushirika wa Majosho hayo ili yanapokuwa yamechakaa yafanyiwe ukarabati mapema iwezekanavyo.

"Undeni ushirika wa kusimamia Majosho haya,ili kila Mfugaji anapokuja kuogesha Ng'ombe wake aweze kuchangia fedha kiasi kidogo ili josho linapoharibika liweze kukarabatiwa kwa fedha ya ushirika huo inayochangiwa na Wafugaji".Alisema.

Mhe.Mpina amesema kuwa,kwa Muda mrefu Rasilimali ya Mifugo hapa nchini haijatendewa haki, amesema kuwa, kuna Migogoro ya Wafugaji na watumiaji Ardhi wengine ya Muda mrefu lakini haijatatuliwa,Wafugaji kufukuzwa kila wanapoenda na Maeneo mengi ya Wafugaji yamebadilishwa Matumizi.

Waziri wa Mifugo Mhe. Luhaga Mpina amesisitiza kuwa hiyo Migogoro inatengenezwa na kuchochewa na Watumishi wa Umma wasiokuwa waaminifu na kusingizia kutekeleza sheria. Amesema kuwa kama ni sheria ya hifadhi itekelezwa lakini kwa kuangalia pia sheria za Mifugo zinasemaje,hatuwezi kukaa kimya tunapoona Mifugo inawekwa Lokapu na inakufa.

"Mifugo hii ni rasilimali ya Taifa, wasomi wengi unaowaona leo, Wamesomeshwa na Mifugo,wanyama hawa walindwe kwasababu wanalima na kufanya shughuli mbalimbali za kijamii."Alisema Mpina.

Aidha,Mhe.Mpina amesema kuwa Jumla ya Ekari 972,500 za Ardhi zimetengwa kwa ajili ya kuwagawia wafugaji wanaozunguka na Mifugo yao na hawana mahali pa kuchungia, amesema kuwa mpaka sasa katika Ranchi ya kalambo, jumla ya Ekari 25,000 zimeshatengwa na tayari Ng'ombe 3,000 wameshaanza kuchungia katika eneo hilo.

Awali Mhe.Luhaga Joelson Mpina alikabidhiwa Madawa ya kuogeshea Mifugo na Mkurugenzi wa kampuni ya Farm Base Bw.Salim Mselem jumla ya lita 8,806.25 kwa ajili ya kusambazwa nchi nzima.

Katika hatua nyingine Waziri Mpina ametoa maagizo kwa wahusika mbalimbali ili kuhakikisha sekta ya Mifugo inakua na kuchangia katika pato la taifa kama ifuatavyo:

Moja, zoeli hili la Uogeshaji Mifugo lisimamiwe na Watumishi wa Umma katika Halmashauri zote nchini.

Pili,Majosho yote ambayo hayafanyi kazi katika Halmashauri mbalimbali nchini yakarabatiwe,na ifikapo mwezi wa sita 2019 kama hayajakarabatiwa nitafuta ushuru wa Rasilimali za Mifugo katika Hamashauri hizo.

Tatu,niliahidi kuwateua Madaktari wa Mikoa na Wilaya wa Mifugo,Nimetengua kauli yangu kwa sababu hawawatei Wafugaji katika maeneo yao.

Na mwisho,Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato naomba mwonyesheni Mwekezaji Eneo la Kujenga kiwanda cha Nyama hapa Chato ili mwezi wa tatu 2019 nije niweke jiwe la msingi ili Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aje azindue Desemba 2019.

.