WAWEKEZAJI WAOMBWA KUWEKEZA KATIKA MALISHO YA MIFUGO

Imewekwa: Sunday 23, May 2021

Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel amewaomba wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza katika malisho ya mifugo kwa sababu kuna fursa kubwa na watasaidia kutatua changamoto ya malisho nchini.

Prof. Ole Gabriel alisema hayo wakati alipoenda kuangalia majani ya malisho ya mifugo yaliyoboreshwa yanayoitwa Juncao yaliyopandwa katika Kitalu kilichopo kwenyeKituo cha Mtandao wa Afya na Elimu cha Kairuki kilichopo Jijini Dar es Salaam Mei 9, 2021.

Akiwa katika Kituo hicho, Prof. Ole Gabriel aliwaomba wawekezaji kuona malisho kama fursa adimu na ya pekee kwa sababu majani ya Juncao yanafaida zaidi ya moja na hivyo itawawezesha wawekezaji hao kutanua wigo wao wa biashara lakini pia watasaidia kutatua changamoto ya malisho nchini.

"Huu ni wakati mzuri kwa wawekezaji kuona hii ni fursa pekee kuwekeza katika malisho kwa sababu itawapa faida zaidi ya moja, hivyo wasiishie katika kuwekeza katika biashara nyingine tu, wafikirie kwamba kuwekeza katika malisho ni uwekezaji unaolipa na tayari soko lipo,"alisema Prof Ole Gabriel

Aidha, Prof. Ole Gabriel amewata Wafugaji kubadirika katika ufugaji wao kwa sababu Serikali inafanya kila jitihada kuboresha ufugaji wao hivyo wawe tayari kutumia teknolojia katika ufugaji wao.

"Wafugaji watambue kwamba Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais, Samia Suluhu Hassan inafanya kila linalowezekana kuongeza kasi ya mabadiriko katika masuala yote ya sekta ya mifugo," aliongeza Prof. Ole Gabriel

Prof. Gabriel alisema kuwa lengo la Serikali ni kuona kuwa changamoto ya malisho nchini inafika mwisho na Wafugaji wanakuwa na malisho bora na ya uhakika kwa mifugo yao.

Naye Mshauri, Mtandao wa Afya na Elimu wa Kairuki, Nganyirwa Karoma alisema kwa kuwa Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeyatambua majani ya Juncao anaamini kuwa hatua hiyo itafanya majani hayo kusambazwa kwa Wafugaji nchi nzima na yatasaidia kutatua changamoto ya malisho.

"Majani haya yana faida nyingi kando ya kutumika kama malisho ya mifugo, pia ni mazuri kwa kutengezea Uyoga na kuzalisha nishati, hivyo hii ni fursa pia kwa Vijana," alisema Karoma

Alisema wao kama shirika watafurahi kuona kuwa majani hayo ya Juncao yanasaidia kubadirisha na kuboresha maisha ya watu hapa nchini.

.