Nifanyeje?
- Zipi sifa za kuorodheshwa kama msaidizi wa mtaalam wa mifugo? (Enlisted Paraprofessional Assistant)
- Zipi sifa za kujiandikisha kama mtaalam msaidizi wa mifugo? (Enrolled Paraprofessional).
- Daktari wa mifugo asiye mtanzania (Foreigner) anasajiliwa vipi na Baraza.
- Daktari wa mifugo asiye Mtanzania anaweza kusajiliwa na kufanyakazi hapa nchini? (Temporary and permanent registration)?
WAVUVI KUANZA KUTUMIA MFUMO WA KUTAMBUA SAMAKI MAJINI
Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), inatarajia kuanza kutumia rasmi mfumo wa kuwapatia wavuvi wadogo taarifa ya mahali samaki walipo ili wavuvi hao waweze kuvua kwa tija na kuondokana na uvuvi wa kubahatisha.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) amebainisha hayo (24.10.2023) jijini Dar es Salaam, mara baada ya kufungua rasmi mkutano wa siku tatu kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 40 ya TAFIRI.
Mhe. Ulega amesema Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Dotto Biteko anatarajia kuzindua mfumo huo Alhamisi wiki hii wakati wa kufunga mkutano huo, ambapo amesisitiza ni mfumo muhimu katika kuwawezesha wavuvi wadogo kufanya shughuli za uvuvi wakiwa na taarifa sahihi kwa kutumia simu ya mkononi.
“Maana ya jambo hili ni kwamba wavuvi wanaondolewa kwenye kuwinda samaki ambapo watakuwa wanaenda kuvua samaki wakiwa na taarifa za wapi samaki walipo na umbali gani hivyo kumsaidia mvuvi kujua rasmi muda watakaotumia pamoja na kiwango cha mafuta ya boti zao.” Amesema Mhe. Ulega
Aidha ameitaka TAFIRI kuongeza vivutio vya samaki maeneo mbalimbali ya Bahari ya Hindi na maji mengine ili yavute samaki wengi kuzaliana na kuongeza uzalishaji wa samaki na kuondokana umasikini ili kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla kwa kuwa ni sera ya uchumi wa buluu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TAFIRI Dkt. Ismael Kimirei amesema taasisi hiyo iliyoanza kazi rasmi kufanya utafiti Mwaka 1983, mfumo ambao unatajia kuzinduliwa kwa ajili ya kuwapatia taarifa wavuvi kupitia simu ya mkononi ni utafiti ambao umechukua muda mrefu hadi kufikia hatua ambayo mfumo uko tayari kuanza kutumika.
Ameongeza kuwa utafiti wa mfumo huo umetumia takriban miaka 10 lakini ni miaka yenye faida kwa kuwa sasa mvuvi ataweza kupokea ujumbe kupitia simu yake ya mkononi ya kujua maeneo ambayo kuna samaki.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Zanzibar (ZAFIRI) Bw. Zakaria Khamis amesema kuna baadhi ya tafiti wamekuwa wakifanya pamoja na TAFIRI ili kuongeza utaalamu ikiwemo ya hivi karibuni kuangalia wingi wa samaki wadogo na kwamba matokeo yake yatatoka hivi karibuni.
Hali kadhalika amesema ZAFIRI imewahi kushirikiana na TAFIRI kuangalia ubora na wingi wa dagaa upande wa Zanzibar ili kupata ujuzi zaidi kutoka TAFIRI ambayo inaadhimisha miaka 40 na ZAFIRI ikiwa na miaka minne pekee.
Mkutano wa siku tatu wenye kuadhimisha miaka 40 ya TAFIRI unatarajia kufungwa Alhamis wiki hii na Naibu Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Dotto Biteko.