WATUMISHI WA SEKTA YA UVUVI WAASWA KUWA NA UADILIFU KATIKA UTUMISHI WA UMMA

Imewekwa: Monday 22, June 2020

Watumishi wa sekta ya Uvuvi wameaswa kuwa na uadilifu katika utumishi wa Umma hasa katika kuzingatia sheria,Kanuni na Taratibu za Nchi.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah alipokua akifungua kikao cha Mafunzo ya maadili ya Utumishi wa Umma, yaliyofanyika katika ukumbi wa St. Gasper leo tarehe 18/06/2020.

Dkt. Tamatamah amewasisitiza watumishi kuwa wazalendo katika kazi na kufuata maelekezo yote ya utumishi wa umma na sheria za Nchi.

Lengo la mafunzo hayo ni kuwakumbusha watumishi kutambua majukumu yao ya kiutumishi pamoja na maadili ya utumishi wa umma.

"Mtumishi anapaswa kujua misingi yake ya kazi katika utumishi na kuepuka kuchukua na kupokea rushwa katika kuwaudumia wananchi," alisema Dkt. Tamatamah.

Naye Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma Bwana kutoka TAKUKURU, Joseph Kasongwa Mwaiselo amewaeleza watumishi madhara ya rushwa kwa serikali, na kwamba baadhi ya watumishi wamekuwa wakikumbatia rushwa na kudhani kuwa itawaongezea kipato.

Mwaiselo amesema madhara ya rushwa serikalini ni pamoja na kupunguza ukuaji wa uchumi kwa sababu ina haribu uwekezaji katika uchumi na pia rushwa inapunguza uwezo wa serikali kugharamia huduma za kijamii ikiwamo Afya na Elimu.

Aidha, akinukuu maneno ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa alipo wasilisha hotuba kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio ya Mapato na Matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu mwaka 2016/2017, Mwaiselo amesema "Hatutaweza kufikia uchumi wa kati unaoendeshwa kwa viwanda kama tutaendelea kulea uzembe, uvivu, na kukwepa wajibu wetu".

Watumishi wametakiwa kuacha rushwa kwani rushwa ni adui wa haki na watumushi wanapaswa kupendana na kuacha majungu ambayo yanasababisha kukosekana kwa haki.

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Alex Mfundo amewasihi watumishi kuhakikisha wanafuata maadili ya utumishi wa umma na amewapongeza watumishi kwa kuitikia wito katika mafunzo hayo.

Katika mafunzo hayo, watumishi wameelekezwa juu ya masuala ya maadili ya utumishi wa umma pamoja na mwongozo kuhusu ushiriki wa watumishi wa umma katika uchaguzi mkuu mwezi Oktoba, 2020.

.