​WATANZANIA WAHIMIZWA KUTUMIA BIDHAA ZA NGOZI ZINAZOZALISHWA NCHINI

Imewekwa: Wednesday 30, June 2021

Serikali imetoa wito kwa Watanzania kujenga utamaduni wa kutumia bidhaa za ngozi ambazo zinazozalishwa na Viwanda vya ndani ili kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya sita ya kuwa na uchumi imara unaotegemea Viwanda.

Wito huo ulitolewa na Afisa Biashara Mkoa wa Dar es salaam, ambaye alimuwakilisha Katibu Tawala wa mkoa huo, Thabit Massa katika hafla ya utoaji wa leseni kwa wachunaji wa ngozi kutoka manispaa ya kinondoni, Temeke na Ilala iliyofanyika jijini Dar es Salaam Juni 18, 2021 ambapo alisema kwa sasa bidhaa za ngozi zimekuwa zikizalishwa kwa viwango vikubwa kutokana na kuwepo kwa Viwanda na uwekezaji mkubwa.

Alisema katika mwaka 2019/20 jumla ya vipande vya ngozi millioni 11.77 vinakadiliwa kuzalishwa huku Uzalishaji wa ngozi ukiwa sawa na uvunaji wa asilimia 12.5 kwa Ng'ombe, asilimia 28.0 kwa mbuzi na asilimia 29.0 kwa kondoo.

"Wastani wa Uzalishaji wa ngozi kwa siku ni vipande 31,000 ambapo vinauwezo wa kuzalisha futi za mraba millioni 138.57 kwa mwaka zenye uwezo jozi viatu 55.42,"alisema Massa

Aliongeza kuwa tasnia ya ngozi kwa sasa imekuwa ambapo kwa sasa kuna Viwanda vitano vinavyosindika vinavyosindika ngozi kufikia hatua ya mwisho.

Alitaja viwanda hivyo vikiwa ni pamoja na kiwanda cha ACE Leather cha mkoani Morogoro, Kiwanda cha Leather kilichopo mkoani Kilimanjaro na Kiwanda cha Himo Tannery and Planters ambapo vyote vinauwezo wa kusindika futi mraba 110,000,15000 na 10,000 kwa siku.

Aliendelea kusema kuwa katika kutambua hilo Wizara imefanya tathimini ya ubora wa ngozi katika machinjio yenye wachunaji kwa kutoa mafunzo na kuwapatia leseni.

"Tumefanikiwa kuendesha mafunzo ya wachunaji wa ngozi 432 wa machinjio ya manispaa za Jiji la Dar es salaam mwezi Januari ambapo leo tunawapatia leseni, na pia Wizara imewajengea uwezo wakaguzi na waweka madaraja ya ngozi wa mkoa wa Dar es salaam, Pwani na Morogoro,” aliongeza Massa

Aidha aliwataka wachunaji kuzingatia mbinu mpya za uchunaji bora wa ngozi huku akisisitiza kuwa wasimamizi wa machinjio kuanzia sasa kutoruhusu mtu asiye na leseni kuingia katika machinjio.

Awali Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Uzalishaji na Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Gabriel Bura alisema lengo la kutoa mafunzo na leseni kwa wachunaji ni kuhakikisha bidhaa ya ngozi inaweza kuzalishwa katika viwanda vikubwa.

Alisema kwa sasa viwanda vinahitaji ngozi zenye kukidhi viwango hivyo kutambulika kwa wachunaji wa ngozi kutasaidia kwa kiasi kikubwa uzalishaji kuongezeka.

"Tafiti zinaonesha kuwa asilimia 45 hadi 65 ya wachunaji wa ngozi wamekuwa wakichagia uharibifu wa ngozi hivyo tumeona kundi hili ni muhimu kulipa mafunzo Kama haya," alisema Bura

Salumu Abdallah ni mmoja wa wachunaji wa ngozi waliopata leseni amesema mafunzo aliyoyapata yatamsaidia kwa kiasi kikubwa kufanya kazi yake kwa viwango vya ubora tofauti na awali.

.