​WANUFAIKA WA MIKOPO YA UFUGAJI SAMAKI WAPATIWA MAFUNZO

Imewekwa: Monday 26, June 2023

Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Mhe. Erasto Sima amewataka wanufaika wa mikopo ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba kuhakikisha wanazingatia mafunzo ya utekelezaji wa miradi hiyo kitaalam ili iweze kuwaletea maendeleo na kuweza kurejesha mikopo kwa wakati

Mhe. Sima alisema hayo Juni 14 mwaka huu wakati akifungua mafunzo kwa vikundi, vyama vya ushirika na watu binafsi wanaotarajiwa kunufaika na mkopo wa masharti nafuu usio na riba ukijumuisha pembejeo za vizimba, chakula cha samaki na vifaranga vya samaki Mkoani Kagera

Aliseme lengo la Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutoa mikopo hiyo ni kutatua changamoto iliyopo kwa wananchi husasani ukosefu wa mitaji na upungufu wa samaki ziwani.

"Hakikisheni mnazingatia utaalamu katika usimamizi, mbegu bora ya samaki mtakaopandikiza, ulishaji wa samaki kwa kutumia chakula bora, ulinzi wa vizimba na biashara kwa kuzingatia taarifa za soko" alisema Mhe. Sima

Aidha alibainisha kuwa Serikali imeshatenga maeneo yanayofaa kwa ajili ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba ambayo ni pamoja na eneo la Rubafu lililounganisha Wilaya ya Bukoba na Missenyi, eneo la Kitua na Ihumbo kisiwa na Bumbire Wilaya ya Muleba

Alitaja maeneo mengine ni Kabasharo, kabwinyora, Mazinga, Ikuza na Nyakabango yote ya Wilaya ya Muleba ambapo vibali vyote TAFIRI, NEMC na Mamlaka ya bonde la ziwa Victoria vimeshatolewa

"Tunategemea maeneo haya yatakuwa mfano wa kuigwa katika uzalishaji wa samaki kwa njia ya vizimba, msisitizo umewekwa kuhakikisha kuwa tunafanya ufugaji endelevu na wenye tija kwa maslahi makubwa ya nchi yetu na wananchi kwa ujumla" alisema Mhe. Sima

Aidha aliwakumbusha wakurugenzi na maafisa Ugani katika Sekta ya Uvuvi kuendelea kutekeleza majukumu yao hasa katika kuwasaidia wanufaika wa mikopo kwa kuwatembelea, kuwapa elimu, kuwashauri na kutatua changamoto watakazo kumbana nazo wakati wa upandikizaji wa samaki, ulishaji na masoko ya samaki.

.