​WANAWAKE WANAOJIHUSISHA NA UVUVI WATAKIWA KUWA WABUNIFU

Imewekwa: Wednesday 30, June 2021

Wanawake wanaojihusisha na shughuli za uvuvi wametakiwa kuwa wabunifu ikiwa ni pamoja na kujengeana uwezo Ili kukuza biashara zao huku wakikumbushwa kujilinda dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi.

Ushauri huo umetolewa leo (24.06.2021) na Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Mara, Bi. Neema Ibamba katika warsha ya siku tatu ya wadau hao Mjini Musoma Mkoani Mara.

Ibamba amesema kuwa biashara yoyote inahitaji ubunifu na kwamba wadau hao kutoka Mikoa ya Kanda ya ziwa lazima waende na wakati.

Aliongeza kuwa ubunifu unaotakiwa ni pamoja na kuwa na vifungashio vizuri vya kisasa kwa ajili ya bidhaa zao pamoja na kuangalia fursa nyingine za masoko zinazowagusa.

Aidha katika kukuza kipato cha familia, Ibamba amewataka wanawake kuendelea kushirikiana na waume zao badala ya kuwadharau kutokana na kipato wanachopata.

"Biashara ama kupata kipato kisiwe kigezo cha kufanya dharau kwa wanaume wenu kwa kuwa mna pesa, hakikisheni kile mnachokipata mnakiweka mezani ili kiwasaidie," alisema Ibamba.

Aidha Ibamba amewataka wanawake hao kujua mbinu mbalimbali za kuweza kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi hususani katika mialo ya kuuzia samaki na dagaa na

kuwaasa kuendelea kushikamana kwa umoja wao Ili waweze kupiga hatua kwenye biashara zao kwa sasa na siku zijazo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo (EMEDO), Bi.Editrudith Lukanga amesema kuwa ushirikiano ndiyo njia pekee ya kuwafikisha wanawake katika mafanikio.

Lukanga amewataka wanawake hao kuendelea kushirikiana na waume zao Ili kulinda ndoa zao badala ya kuwa chanzo cha migogoro katika ndoa hizo.

Lukanga ameongeza kuwa shirika lao limekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha Umoja wa Wanawake wanaojihusisha na Uvuvi (TAWFA) unazidi kuimarika na kuhusisha kundi kubwa.

Kwa upande wake, Afisa Uvuvi Mwandamizi ambaye pia ni mratibu wa dawati la jinsia la Uvuvi la Wizara kutoka Wizara ya Mifugo na Uvivi, Bi. Upendo Hamidu amesema kuwa Wizara hiyo itahakikisha inaweka mipango imara Ili kuwasaidia wanawake katika shughuli zao.

Warsha hiyo ya siku tatu imeandaliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Shirika la EMEDO na kufanyika mjini Musoma mkoani Mara.

.