VIONGOZI WAANDAMIZI WA WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI WAKAGUA UTENGENEZAJI WA BOTI ZA UVUVI ZANZIBAR.

Imewekwa: Thursday 13, April 2023

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe Pamoja na Naibu Katibu Mkuu Uvuvi, Agness Meena, jana tarehe 6 Mach, 2023 wamekagua utengenezaji wa Boti za kisasa za uvuvi aina ya fiber zinazotengenezwa na kampuni ya Qiro Group Limited ya zanzibar.

Kampuni ya Qiro Group Limited inatengeneza Jumla ya Boti Mia moja na kumi nane (118) zenye urefu wa Mita tofauti tofauti.

Prof.Shemdoe amesema kuwa ameridhishwa na kasi ya utengenezaji wa Boti hizo, hivyo amemwelekeza Mkandarasi huyo kufanya kazi kwa bidii ili kukamilisha boti hizo kwa muda uliopangwa.

"Leo nimekuja hapa Zanzibar na Naibu Katibu Mkuu Uvuvi, Mama Agness Meena pamoja na baadhi ya wakurugenzi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kwa lengo la kukagua utengenezaji wa boti hizi Mia moja kumi na nane (118). Boti hizi zikikamilika zitakabidhiwa kwa walengwa ambapo zitachochea ukuaji wa uchumi na kipato cha mwananchi mmoja mmoja." Alisema Prof. Shemdoe.

Aidha, Boti zinazotengenezwa na kampuni ya Qiro limited zinaurefu mita tofauti tofauti, zikiwemo Boti mita 14 ambapo idadi yake ni 11, Boti mita 12 idadi yake ni 39, Boti mita 10 idadi yake ni 40 na Boti mita 5 idadi yake ni 28.

Prof. Shemdoe amemshukuru sana Dkt.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwakuwa mstari wa mbele katika kutengeneza na kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi wake ili kukuza uchumi wa buluu

"Namshukuru sana Mhe. Rais kwakuwa Mstari wa mbele bila kuchoka, kutengeneza mazingira Wezeshi kwa wananchi. Kwa sababu boti hizi zikikamilika zitakabidhiwa kwa wavuvi wadogo wadogo, hii inamaana kwamba wavuvi hawa sasa watashiriki kikamilifu katika mnyororo wa thamani katika Sekta ya uvuvi nchini Tanzania." Alisema Prof. Shemdoe.

Hali kadhalika, Prof. Shemdoe amesema kuwa wakandarasi wote wanaotekeleza Miradi mbalimbali ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakae tayari, maana atafanya ziara za kushitukiza katika ukaguzi wa Miradi hiyo

.