Nifanyeje?
- Zipi sifa za kuorodheshwa kama msaidizi wa mtaalam wa mifugo? (Enlisted Paraprofessional Assistant)
- Zipi sifa za kujiandikisha kama mtaalam msaidizi wa mifugo? (Enrolled Paraprofessional).
- Daktari wa mifugo asiye mtanzania (Foreigner) anasajiliwa vipi na Baraza.
- Daktari wa mifugo asiye Mtanzania anaweza kusajiliwa na kufanyakazi hapa nchini? (Temporary and permanent registration)?
ULEGA: MAONO YA RAIS DKT, SAMIA KUIFANYA MSOMERA KUWA KIJIJI CHA MFANO YATATIMIA
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema serikali ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kukifanya Kijiji cha msomera kuwa cha mfano kwa ufugaji na ndio maana imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kujenga na kuboresha miundombinu ili wafugaji waweze kufanya ufugaji wenye tija zaidi.
Waziri Ulega alisema hayo wakati wa ziara yake aliyoifanya katika Kijiji cha Msomera, Wilayani Handeni Mkoani Tanga leo Septemba 13, 2023 ambapo alipata fursa ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya mifugo ikiwemo mabirika ya kunyweshea mifugo mashamba darasa la malisho na visima vya maji.
Alisema kuwa Wizara yake kwa sasa itajielekeza katika kuondoa vichaka ili wafugaji waweze kulima malisho, watajenga maghala kwa ajili ya kuhifadhia hayo malisho, kujenga mabwawa, kuchimba visima na kujenga majosho ili wafugaji waweze kufuga kisasa, mifugo inenepeshwe ili waweze kupata kipato kizuri zaidi.
Akiongea na wafugaji waliopo katika Kijiji hicho cha Msomera, Mheshimiwa Ulega alisema kuwa maono ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kukifanya Kijiji cha msomera kuwa Kijiji cha mfano ili wafugaji wanaofanya shughuli zao katika maeneo mengine waweze kujifunza na hatimae kuingia katika ufugaji wa kisasa na wenye tija zaidi.
“Mimi nataka niwahakikishieni kwa mwendo tunaokwenda nao sina shaka, naona kabisa nia ya Mhe. Rais ya kuifanya Msomera kuwa Kijiji cha mfano katika ufugaji litafanikiwa,na hilo tutalisimamia,”alisema Mhe. Ulega
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Albert Msando alisema kuwa wao kama Serikali ya Wilaya wako tayari kushirikiana na Wizara katika kufanikisha upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi wa Kijiji cha Msomera ili waweze kuendesha vizuri Maisha yao ya kila siku kama serikali ilivyokusudia.
Naye, aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mzee Saning’o Ole Telele alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha Kijiji hicho cha msomera, huku akiiomba serikali kutorudi nyuma katika zoezi hilo la kuhamishia watu katika Kijiji cha msomera ili Ngorongoro liendelee kubaki kuwa eneo la mbuga za Wanyama.