ULEGA AWATAKA WATAALAMU KUONGEZA UBUNIFU KUKUZA SEKTA ZA MIFUGO NA UVUVI

Imewekwa: Wednesday 01, November 2023

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amewataka Wataalam wa Sekta za Mifugo na Uvuvi kuongeza ubunifu katika shughuli zao za kila siku ili mchango wa sekta hizo katika uchumi wa Taifa uweze kuongezeka tofauti na ilivyo sasa ambapo sekta ya uvuvi inachangia asilimia 1. 8 na sekta ya mifugo inachangia asilimia 7.0.

Waziri Ulega ameyasema hayo wakati akifungua Kongamano la 46 la Uzalishaji na Uendelezaji wa Mifugo na Mkutano Mkuu wa 47 wa Mwaka wa Chama cha Wataalamu wa Uzalishaji na Uendelezaji wa Mifugo na Uvuvi (TSAP) linalofanyika katika Ukumbu wa Olasit Garden, Arusha leo Oktoba 25, 2023.

Aliongeza kwa kuwataka Wataalam hao kutambua kuwa wanajukumu kubwa la kuendeleza sekta hizo huku akiwaeleza kuwa huu ni wakati mwafaka wa kufanya mapinduzi makubwa katika minyororo ya thamani ya mifugo na samaki ili kukidhi mahitaji ya chakula na lishe bora ndani na nje ya nchi.

"Wizara ninayoisimamia inatia mkazo kwenu wataalamu muweke nguvu katika taaluma zenu ili kuongeza uzalishaji wa mifugo na samaki kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi", alisema Mhe. Ulega

Aliendelea kufafanua kuwa Tanzania kama mwanachama wa Umoja wa Mataifa, ilishiriki kama mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Mifumo ya Chakula ya Afrika (AGRF) mwaka huu ambapo wadau wote duniani chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa walikubaliana kusimamia Mabadiliko ya mifumo ya chakula na kuongeza uzalishaji na kuhakikisha upatikanaji wa chakula kwa wote.

Hivyo, aliitaka TSAP na wanachama wote kuendelea kuunga mkono makubaliano hayo ambayo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeazimia kuyatekeleza kwa vitendo.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wataalamu wa Uzalishaji na Uendelezaji wa Mifugo na Uvuvi (TSAP), Dkt. Jonas Kizima alisema moja ya malengo ya chama hicho ni kuhimiza maendeleo katika sayansi ya uzalishaji wa mifugo na uvuvi hapa nchini.

.