Ulega ahimiza Wananchi kuchangamkia fursa Sekta ya Mifugo

Imewekwa: Monday 08, April 2024

Ulega ahimiza Wananchi kuchangamkia fursa Sekta ya Mifugo

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amewataka wananchi wanaoishi katika Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ikiwemo Iringa na Njombe kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta ya mifugo hususan ufugaji wa ng’ombe wa maziwa.

Waziri Ulega ametoa wito huo mapema leo Aprili 7, 2024 wakati akihitimisha tukio la Mashindano ya Kumi ya Kuhifadhi Qur’an Nyanda za Juu Kusini yaliyoandaliwa na taasisi ya Dhi Nureyn ya mkoani Iringa.

“Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo mahususi katika Wizara yangu ya kuhakikisha sekta ya mifugo inainuka na kusaidia watanzania kupitia fursa mbalimbali ambazo yeye ameendelea kuzitoa katika sekta hiyo kila uchao”, alisema

Aliongeza kwa kusema kuwa katika mwaka ujao wa fedha (2024/2025), wizara yake imejipanga kuongeza uwekezaji kwenye tasnia ya maziwa ambapo watatoa ng’ombe wa maziwa wa kisasa kwa vikundi na kujenga vituo vidogo vya kukusanyia maziwa zaidi ya 700 na vikubwa visivyopungua 100 ili maziwa mengi yapatikane na kupelekwa viwandani kwa ajili ya kuchakatwa.

“Katika mkoa huu wa Iringa kuna viwanda vya kuchakata Maziwa vya Asas na Shaffer ambavyo vinahitaji maziwa, jipangeni kufanya kazi ya uzalishaji wa maziwa muweze kupeleka katika viwanda hivyo ili uchumi upatikane kwenu na Taifa kwa Ujumla,” alibainisha

Aliendelea kufafanua kuwa fursa hizo ni kwa wananchi wote hususani kina mama na vijana, hivyo wajipange na kujiandaa kupokea fursa hizo zinazotolewa na serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

.