​TUSISUBIRI KUSUKUMWA, TUFANYE KAZI - Prof. Ole Gabriel

Imewekwa: Wednesday 01, September 2021

Katibu Mkuu wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel amewataka watumishi wote wa Sekta yake kutosubiri kushinikizwa ili watimize wajibu wao.

Prof. Ole Gabriel ameyasema hayo leo (06.08.2021) alipokutana na watumishi hao kwa lengo la kutathmini mipango na malengo mbalimbali yanayotarajiwa kutekelezwa na sekta hiyo kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

“Tusisubiri kusukumwa, wakurugenzi na wakuu wa vitengo simamieni hilo na kuhakikisha watu wenu wa chini wanatimiza wajibu wao ipasavyo” amesema Prof. Ole Gabriel.

Prof. Ole Gabriel amewaahidi watumishi hao kuwa katika mwaka huu wa fedha Sekta yake itaendelea kuboresha mazingira yao ya kazi na kuwaongezea morali ya kufanya kazi.

“Watu wengi sana wanahamia kwenye Sekta yetu kwa hivi sasa na tunawakaribisha sana na wale wanaotaka kuhama walete maombi yao nami ntapitisha haraka sana ila nawakumbusha kuwa pindi wakitaka kurejea mchakato huo hautakuwa mwepesi” Amesisitiza Prof. Ole Gabriel.

Katika hatua nyingine Prof. Ole Gabriel amewataka watendaji na watumishi wote wa sekta yake kuchukua tahadhari ya kutosha ili kujikinga na maambukizi ya wimbi la tatu la virusi vya Uviko 19.

“Hofu haitakufikisha popote na ukishaanza kuwa na hofu hata kinga za mwili wako zitapungua hivyo msijenge hofu na wala msibaguane” Ameongeza Prof. Ole Gabriel.

Prof. Ole Gabriel amewataka watumishi hao kupuuza taarifa zinazotolewa na vyanzo visivyo rasmi na kutafuta ukweli wa masuala yote yanayohusiana na maambuzi ya virusi hivyo kupitia vyanzo rasmi vilivyofanya utafiti kuhusiana na jambo hilo.

“Hatobaguliwa mtumishi yoyote aliyechanja au ambaye hajachanja kwa sababu suala la chanjo ni la hiyari na hatolazimishwa yoyote kufanya hivyo lakini ni vizuri uwe na sababu za msingi za kutochanja” Amesema Prof. Ole Gabriel

Kikao hicho baina ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel na watumishi wa sekta hiyo ni sehemu ya utamaduni wa Viongozi mbalimbali wa Wizara hiyo kukutana na watendaji na watumishi waliopo chini yao ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya Wizara hiyo.

.