SERIKALI YAWEKA NGUVU KATIKA UTAFITI WA RASILIMALI ZA BAHARI NCHINI ILI KUWA NA UVUVI ENDELEVU

Imewekwa: Thursday 20, July 2023

Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Serikali ya Norway imepokea meli ya utafiti ya Dr. Fridtjof Nansen ambayo inafanya utafiti wa ikolojia ya Bahari na rasilimali za uvuvi zinazopatikana katika Bahari ya Hindi na kusaidia kuimarisha usimamizi wa Rasilimali za Bahari.

Akiongea, katika hafla ya kuipokea rasmi meli hiyo katika Bandari ya Dar es salaam leo 11 Julai 2023, Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi wa Serikali ya Zanzibar, Mhe. Suleiman Makame, amesema utafiti huo unafanyika Tanzania Bara na visiwani (zanzibar) na utatoa taswira ya aina za samaki wanaopatikana baharini kwa ajili ya kuweka mipango madhubuti ya usimamizi. Utafiti huo, umeanza kufanyika 28 Juni 2023 na utakamilika 28 Julai 2023.

"Tumekuwa tukifanya uvuvi bila kujua ni aina gani ya samaki na viumbe wengine wa Bahari tulionao, kwa hiyo tutakapokuwa na takwimu sahihi za rasilimali za samaki waliomo baharini tutaweka mkakati wa kudhibiti mazao ya baharini hasa aina za samaki ambao wamekaribia kutoweka." amesema Makame.

Mhe. Makame amesema ni mara ya tatu utafiti kama huu unafanyika katika eneo la bahari nchini Tanzania, kwa mara ya kwanza ulifanyika mwaka 1982, mara ya pili ukafanyika mwaka 2018 na sasa unafanywa mara ya tatu na meli ya Dr Fridtjof Nansen.

Amesema baada ya kukamilika kwa utafiti huo Julai 25 mwaka huu Serikali itafahamu aina za samaki waliomo Baharini na tumeambiwa kuna aina mpya za samaki ambao hawajawahi kuonekana lakini kupitia utafiti huu, aina hizo zitawekwa katika rekodi ya dunia.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI) Dkt. Ismael Kimerei amesema utafiti unaofanyika ni muhimu katika kupata uhalisia wa kiasi cha samaki waliopo katika maji Baharini.

"Hadi sasa kiasi cha samaki kinachokadiliwa kuwemo katika maji ya ni tani 100,000 utafiti huu ulifanyika 1982, takwimu za 2018 hazitumiki kwasababu hazikuwa sawa,

"Tunaamini utafiti unaokwenda kufanyika sasa utatoa majibu sahihi na tutayasilisha Wizarani kwa ajili ya matumizi ya Wizara ikiwemo utungaji wa Sera ,"amesema Kimerei.

Dkt. Kimerei amesema katika meli hiyo wapo watafiti 25 wakiwamo 13 kutoka Tanzania.

Kwa upande wake Mwakilishi mkazi wa Shirika la FAO Tanzania Dkt. Nyabenyi Tito Tipo amesema, wanatambua umuhimu wa kusaidia ukuaji wa sekta ya uvuvi Tanzania hivyo wataendelea kuishika mkono Serikali na kushirikiana na wadau wengine kuendeleza rasilimali za bahari.

Amesema takwimu zitakazopatikana kwenye utafiti huo zitakuwa hazina ya Tanzania. Meli hiyo ya utafiti imejumuisha watafiti kutoka Kenya, Msumbiji Afrika kusini, Australia na Norway

Tanzania inakusudia kuwa na takwimu za rasilimali zilizopo baharini pamoja na kuweka mkakati wa uvuvi kwa lengo la kudhibiti shughuli za uvuvi na ulinzi wa rasilimali za samaki walio hatarini kutoweka vilivyo hatarini kutoweka. hii ni baada ya kuruhusu Serikali ya Norway pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Chakula(FAO) kuanza utafiti wa rasilimali zilizopo baharini kwa Tanzania bara na visiwani

.