SERIKALI YATEKETEZA TANI 11 ZA SAMAKI ZENYE THAMANI YA Sh.MIL 66

Imewekwa: Wednesday 13, March 2019

SERIKALI YATEKETEZA TANI 11 ZA SAMAKI ZENYE THAMANI YA Sh.MIL 66

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeteketeza Tani 11 za samaki zenye thamani ya zaidi ya Tshs mil.60 zilizobainika kuwa na sumu na hazifai kwa matumizi ya binadamu.

Tukio hilo la uteketezaji wa samaki wenye sumu limefanyika leo likiongozwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mh.Luhaga Joelson Mpina (Mb) katika eneo la dampo lililopo Pugu Kinyamwezi Jijini Dar es Salaam.

Hatua hiyo imefikiwa na serikali baada ya Mahakama kuridhia kuwa samaki hao walioingizwa nchini si salama kwa matumizi ya binadamu.

“Lengo ni kuhakikisha rasilimali za uvuvi zinakuwa endelevu, zinavuliwa salama ili ziendelee kuwepo katika kizazi cha sasa na kizazi kijacho, ”alisema Mh.Mpina.

Pia Waziri Mpina alisema, Watanzania wako Salama hakuna namna yoyote mazao ya uvuvi yanaweza kuwafikia yakiwa hayajapimwa na kuthibitishwa.

Aidha Mhe. Mpina amezitaka Taasisi za Serikali zinazohusika na udhibiti na usimamizi wa sekta ya uvuvi kufanya kazi kwa bidii na kushirikiana ili kuhakikisha watanzania wanatendewa haki katika biashara za ndani na nje ya nchi.

“Serikali ya awamu ya tano ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli inahakikisha ipo kwa ajili ya kumlinda Mtanzania asiweze kupata madhara yoyote na kuwa salama”. alisema Mpina.

.