​SERIKALI YAPONGEZA SEKTA BINAFSI KWA KUKUZA SEKTA YA UVUVI

Imewekwa: Friday 25, November 2022

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imelipongeza Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Wanyamapori (WWF) kwa kuviwezesha vikundi saba vya ujasiriamali vya uvuvi kwa jumla ya Shilingi Milioni Thelathini na Tano, pikipiki nne, boti tatu na injini zake, pamoja na makoti 30 ya kujiokoa (life jackets) kwa halmashauri mbili za Wilaya za Kilwa Mkoani Lindi na Kibiti Mkoani Pwani.

Shukrani hizo zimetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Sekta ya Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah katika hotuba yake iliyosomwa na Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji, Bw. Anthony Dadu wakati wa maadhimisho ya siku ya mvuvi duniani yanayokwenda sambamba na Mwaka wa Kimataifa wa Wavuvi Wadogo na Wakuzaji Viumbe Maji 2022 (International Year of Artisanal Fisheries and Aquaculture (IYAFA) yaliyofanyika katika kijiji cha Somanga Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi.

Amesema hatua hiyo itaongeza chachu ya usimamizi bora wa rasilimali za uvuvi utakaopelekea upatikanaji kwa wingi wa mazao ya uvuvi yenye ubora na hivyo kuwezesha jamii kupata lishe bora na kuongeza kipato ikizingatiwa mafanikio katika usimamizi wa rasilimali za uvuvi yanategemea sana vitendea kazi imara.

"Nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mkurugenzi Mkazi wa WWF Dkt. Amani Ngusaru kwa kuendelea kuwajali na kuwawezesha wananchi wetu katika kuimarisha shughuli zao za kiuchumi na hivyo kuleta tija katika maisha yao" alisema Bw. Dadu katika taarifa hiyo.

Aidha amewataka viongozi wa vijiji ambao watanufaika na zana hizo ikiwemo Nyamatungutungu, Marendego, Njia nne, Somanga Kusini, Somanga Kaskazini, Songosongo, Pombwe, Jaja, Kiomboni, Msala, Dongo, Kilindoni, Chunguruma, na Ndagoni kutimiza wajibu wao mkubwa wa kushirikiana kuvitunza vitendea kazi hivyo ili vinufaishe taifa na familia zao.

Hali kadhalika aliwataka wakurugenzi wa halmashauri zote kuhakikisha wanapata taarifa za mara kwa mara juu ya matumizi sahihi na yaliyokusudiwa kupitia vifaa hivvyo.

"Nitoe wito kwa halmashauri husika kuona umuhimu wa kuweka utaratibu mzuri utakaowezesha Vikundi vya Kusimamia Rasilimali ya Uvuvi Mwaloni (BMU) katika halmashauri zenu zinanufaika na vifaa hivi pale wanapohitaji kuvitumia katika maeneo yao." Alisema Bw. Dadu

Aidha amewakumbusha kuwa kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha Sheria ya Uvuvi na Kanuni zake zinazingatiwa hali itakayosababisha waendelee kunufaika na fursa nyingi zilizopo katika sekta ya uvuvi.

Akiwasilisha mada kuhusu dhima ya siku ya mvuvi duniani Mratibu wa Programu ya Bahari na Pwani WWF Dkt. Modesta Medard amesema kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Shirika la Kilimo na Chakula Duniani la Umoja wa Mataifa (FAO) inaonesha zaidi ya theluthi mbili ya samaki wote duniani wamevuliwa kupita kiasi au wamevuliwa wote na zaidi ya theluthi moja wako katika hali ya kupungua.

Amesema sababu ya kupungua huko ni kutokana na kutoweka kwa makazi ya samaki, uchafuzi wa mazingira na ongezeko la joto duniani ambapo siku ya mvuvi duniani inasaidia kutambulisha umuhimu wa sekta ya uvuvi kwa maisha ya binadamu, viumbe maji kwenye mito, maziwa na bahari.

"Samaki wanamchango mkubwa katika uhakika wa chakula duniani ni muhimu kwa lishe bora ya watu wote ulimwenguni hususan kwa jamii zilizopo karibu na mito maziwa na bahari" alisema.

.