SERIKALI YAJA NA MKAKATI WA CHANJO ZA MAGONJWA MUHIMU YA MIFUGO KOTE NCHINI

Imewekwa: Wednesday 16, December 2020

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul ameagiza kuandaliwa kwa mkakati shirikishi wa kupeleka chanjo kwa wafugaji kuanzia mwezi Februari Mwaka 2021 kupitia programu za chanjo ya magonjwa muhimu zitakazosimamiwa na wizara.

Akizungumza (12.12.2020) wakati akifunga kikao cha 38 cha Chama cha Madaktari wa Mifugo Tanzania (TVA) kilichofanyika Mkoani Arusha kuanzia Tarehe 10 hadi 12 Mwezi Desemba Mwaka 2020, ambapo pia amezindua mchanganyiko wa chanjo tatu kwa ajili ya kuku kwenye magonjwa ya mdondo, ndui na mafua ameagiza kuanzishwa kwa uchanjaji wa mifugo ikiwa na lengo kuu la kuhakikisha wizara inasimamia chanjo ya magonjwa yote ifikapo Mwaka 2022.

“Hizi programu zitasimamiwa na wizara na siyo kuiachia halmashauri kwani wao hawana uwezo wa kutekeleza majukumu haya muhimu, hivyo kwa kuwa wizara imeshatayarisha kalenda ya chanjo na bei elekezi licha ya mapungufu machache yaliyopo ninamuelekeza Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo aende na aandae mkakati shirikishi na kupekeleka chanjo kwa wafugaji kuanzia mwezi Februari, mwaka 2021.” Amesema Mhe. Gekul

Aidha, Naibu Waziri Gekul amesema kwa kuzingatia matakwa ya sheria ya Mwaka 2003 serikali inapaswa kuhakikisha ina madaktari wa mifugo katika mikoa na halmashauri kwa kutambua kuwa kwa muda mrefu kumekuwepo na ukosefu wa madaktari wa mifugo kwa mikoa 10 na halmashauri 77 Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na halmashauri husika itawasilisha mapendekezo ya ikama ya watumishi kwa Utumishi kwa ajili ya kuingizwa kwenye bajeti ya mwaka 2012/2022, lengo ikiwa ni kuhakikisha watumishi hawa wanaajiriwa ili kusimamia vizuri tasnia ya wanyama.

Pia, Mhe. Gekul amesema kwa kutambua kilio kikubwa cha watumishi waliojiendeleza kimasomo ambao hawatambuliwi na mfumo wa utumishi kwa kuwa wizara haijaainisha sifa ya mafunzo hitajiwa kwa watumishi wa sekta ya mifugo, tathmini itafanyika ili wizara iainishe mafunzo hitajiwa kwa watumishi wa kada mbalimbali na kuwasilisha utumishi na hivyo wale walio na sifa hitajiwa kufanyiwa marekebisho katika mfumo wa kiutumishi ili kuwaongezea ari ya kufanya kazi.

Kwa kuzingatia changamoto zilizopo katika Sekta ya Mifugo nchini Naibu Waziri Gekul amesema atamshauri Waziri wa Mifugo na Uvui Mhe. Mashimba Ndaki kuunda kikosi kazi kishirikishi kwa ajili ya kuishauri wizara katika masuala muhimu na kumtaka Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Msajili wa Baraza la Vetarinari Tanzania, kuandaa andiko ili liwasilishwe kwa Waziri Ndaki kwa ajili ya kupata ridhaa yake.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari wa Mifugo Tanzania (TVA) anayemaliza muda wake Prof. Dominick Kambarage amesema mfumo wa kusimamia watumishi na Sekta ya Mifugo ni muhimu kuhakikiwa ili kuimarisha sekta hiyo ambapo Mwaka 2019 TVA na TAMISEMI walianzisha mazungumzo kwa kina namna ya kusimamia sekta na watumishi.

Naye Msajili wa Baraza la Veterinari Tanzania Dkt. Bedan Masuruli akizungumza kando ya kikao cha 38 cha Chama cha Madaktari wa Mifugo Tanzania (TVA), amesema baraza limejadili pia maadili kwa wataalam mbalimbali wa mifugo ambao wameshindwa kutoa taarifa za magonjwa kwa idara ya huduma za mifugo kila wiki na kila mwezi, hivyo kulazimika kutoa onyo kali kwa wataalamu 9 juu ya utoaji wa taarifa.

“Tarehe 9 Desemba Mwaka 2020 baraza liliitisha kikao cha dharula kujadili maadili na kushuhudia karibu asilimia 44 ya wataalamu hawatoi taarifa za magonjwa ya mifugo ambapo katika wilaya 184, wataalamu 78 walikuwa wahatoi taarifa lakini baada ya kufanya mahojiano ya awali, wataalamu 34 walibakia kutotoa taarifa ambapo 19 walifika kwenye kikao na walipohojiwa wataalamu 9 walionekana hawana ushahidi wamepewa onyo kali na kuhakikisha katika mwaka mmoja hawakosi kabisa kutoa taarifa za magonjwa ya mifugo kila wiki na kila mwezi.” Amefafanua Dkt. Masuruli

Katika kikao hicho pia Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul amezindua chanjo mpya ya kuku inayotengezwa na wanasanyansi kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), inayodhibiti magonjwa matatu kwa mara moja inayofahamika kwa jina la Tatumoja imefanyiwa utafiti na kutengenezwa na wanasanyansi hao wakiongozwa na Prof. Philemon Wambura na Dkt. Mirende Kichuki.

Chanjo hiyo ina mchanganyiko wa chanjo tatu kwa ajili ya kudhibiti magonjwa ya mdondo, ndui ya kuku na mafua ya kuku na kwamba itakuwa na faida kwa kuweza kutunzwa na kutumika katika joto la kawaida bila kuhitaji ubaridi wa jokofu.

.