Nifanyeje?
- Zipi sifa za kuorodheshwa kama msaidizi wa mtaalam wa mifugo? (Enlisted Paraprofessional Assistant)
- Zipi sifa za kujiandikisha kama mtaalam msaidizi wa mifugo? (Enrolled Paraprofessional).
- Daktari wa mifugo asiye mtanzania (Foreigner) anasajiliwa vipi na Baraza.
- Daktari wa mifugo asiye Mtanzania anaweza kusajiliwa na kufanyakazi hapa nchini? (Temporary and permanent registration)?
SERIKALI YAGAWA VIFARANGA 2600 KWA VIKUNDI VYA KINAMAMA MKURANGA

Katika jitihada za kuwakwamua kiuchumi wananchi hususan kinamama, Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imegawa Vifaranga 2600 kwa mashamba darasa mawili katika kata ya Vikindu na Kimanzichana vilivyopo wilayani Mkuranga, mkoani Pwani.
Akizungumza mara baada ya kugawa vifaranga hivyo Novemba 9, 2021, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Idara ya utafiti na mafunzo, Dkt. Hassan Mruttu alisema vifaranga hivyo vitakaa katika mashamba hayo kwa wiki nne kabla ya kusambazwa katika vikundi 17 vya Wilaya hiyo.
Alisema pamoja na kuwepo kwa vifaranga hivyo, pia vikundi hivyo vitapewa chakula cha kuvikuza pamoja na wataalamu wa kusaidia ukuaji wa kuku katika Wilaya hiyo.
"Tumepokea vifaranga 2600, tumegawa katika mashamba darasa mawili katika kikundi cha Kisawani na kikundi cha tujikomboe hivi vitakaa hapa kwa wiki 4 na baadaye tutavisambaza kwa vikundi 17, ili kuwasaidia wakinamama kujikwamua kiuchumi," alisema Dkt. Mruttu
" Kuna tofauti kubwa kati ya mashamba ya mfano na mashamba darasa, hili ni shamba darasa, kwanzia Novemba 10, wataalamu watakuwa hapa na baada ya hapa tu nategemea wana kikundi wa vikundi hivi viwili mkawe waalimu kwa vikundi hivyo vingine 17,"alisema
Kwa upande wake Afisa mifugo na uvuvi wa Wilaya hiyo Bi. Anna Kiria aliwataka wanakikundi kuongeza umakini katika kufuatilia mafunzo ili kuleta matokeo chanya katika uzalishaji.
"Vifaranga hawa wanaitaji usafi wa kutosha, umakini na kujitolea, tutapewa mafunzo tuzingatie, na mwisho tutapewa vyeti vitakavyotufanya na sisi kwenda kuwafundisha wenzetu," alisema Anna
Alisema halmashauri hiyo itafuatilia kwa ukaribu kuona kila mmoja anatimiza wajibu wake, na haitamvumlia mwana kikundi atakayekuwa sababu ya kukwamisha shughuli hiyo ya maendeleo.
Aidha mwenyekiti wa kikundi cha Kisawani kata ya Vikindu, Bi. Sintaweza Omary, aliipongeza serikali ya awamu ya sita huku akiiomba kuongeza jitihada katika kuwasaidia wakinamama vijijini.
"Mradi huu utaenda kukuza uchumi wa wakinamama wa Mkuranga, hivyo tunamshukuru Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hasan kwa kuwa kumbuka wakinamama na tunamuomba asichoke katika kuhakikisha wanajikwamua kupitia asilimia 10 zitolewazo katika halimashauri, "alisema