SERIKALI KUBORESHA ZAIDI MAZINGIRA KWA WADAU WA KUKU

Imewekwa: Wednesday 01, November 2023

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti amesema wizara ina jukumu la kurahisisha shughuli za wadau wa tasnia ya kuku na wadau wengine wa sekta za mifugo na uvuvi huku akiwataka wadau hao kuhakikisha wanasimamia usalama wa mazao yanayotokana na mifugo yao.

Naibu Waziri Mnyeti amebainisha hayo (13.10.2023) jijini Dar es Salaam, wakati akifungua rasmi Maonesho ya Kuku na Ndege Wafugwao kwa Mwaka 2023 ambapo amesema serikali ipo tayari kupokea changamoto mbalimbali zinazowakumba wadau wa sekta za mifugo na uvuvi na kuzitafutia ufumbuzi.

Aidha, amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi haipo tayari kuona watu wanaofanya kazi kinyume na utaratibu ikiwemo kuingiza vifaranga nchini kinyume na sheria ambapo ni kuhatarisha afya za walaji na kusababisha hatari ya magonjwa ya mlipuko ukiwemo wa mafua ya ndege, hivyo kuainisha kuwa wizara itahakikisha inazidi kuzuia njia zote zisizo rasmi na watu ambao wanaingiza vifaranga nchini kinyume na sheria kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Wizara haiko tayari kuteketeza vifaranga vinavyoingizwa nchini kinyume na sheria, bali itaweka mkakati wa kuhakikisha hakuna mwanya wa kuwezesha mtu yeyote kuingiza vifaranga hivyo na endapo akibainika, atachukuliwa hatua za kisheria.” Amefafanua Mhe. Mnyeti

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Dkt. Daniel Mushi amekipongeza Chama Kikuu cha Wafugaji wa Kuku Tanzania (PAT) na vyama vyake mwambata kwa kuwa vimekuwa imara katika kusimamia tasnia ya kuku na vimekuwa vikishirikiana na wizara katika masuala mbalimbali ili kukuza tasnia hiyo.

Dkt. Mushi amesema ni wakati sasa wa vyama vingine vya mifugo kuiga mfano huo kuhakikisha tasnia za mifugo wanazozisimamia zinakuwa na nguvu zaidi na kuibua hoja zenye tija kwa ajili ya kukuza tasnia hizo.

Naye Mwenyekiti wa PAT, Bi. Florence Maximambali amegusia changamoto mbalimbali ambazo wanakabiliana nazo ikiwemo ya bei za nafaka kwa ajili ya vyakula vya kuku yakiwemo mahindi hivyo kuiomba serikali kuwa na ghala maalum la kuhifadhia mahindi kwa ajili ya mifugo pamoja na matumizi ya mahindi ya njano.

Pia ametaja ukosefu wa soya ambayo zaidi inaagizwa kutoka nje ya nchi nayo inachangia katika kuongeza gharama ya uandaaji wa vyakula vya kuku hivyo kuiomba serikali kuweka msisitizo wa uwepo wa kilimo cha zao hilo kwa wingi.

Maonesho ya Kuku na Ndege Wafugwao kwa Mwaka 2023 yanye kauli mbiu Kuku na Mayai Protini Bora yanaenda sambamba na Maadhimisho ya Siku ya Ulaji Yai Duniani ambapo Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti amekabidhi makasha yenye mayai kutoka kwa Chama cha Wafugaji wa Kuku wa Mayai Tanzania (PFAT), kwa ajili ya vituo vinne vya watoto yatima vilivyopo jijini Dar es Salaam ili kuhamasisha ulaji wa mayai kwa watoto na watu wazima, huku Mwenyekiti wa Chama cha Mazingira na Ufugaji Tija Tanzania (CHAMAUTA) Bw. Jeremiah Wambura amekabidhi fedha Shilingi Laki Tatu kwa ajili ya vituo vya watoto yatima ili vinunue mchele.

.