​SASA NAONA MAONO YA DKT. SAMIA KUPITIA SEKTA YA MIFUGO YANATIMIA-DKT. MPANGO

Imewekwa: Thursday 13, April 2023

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kasi kubwa aliyoiona kwa upande wa sekta ya Mifugo.

Mhe. Dkt. Mpango amebainisha hayo Aprili 12, 2023 mara baada ya kufika kwenye eneo la Shamba la Mifugo la Mabuki lililopo Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza alikotembelea na kukagua Mpango wa Mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana kupitia miradi ya unenepeshaji wa Mifugo unaotekelezwa katika vituo vya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) na Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) vilivyopo shambani hapo.

"Mhe. Rais alikuwa analalamika sana kuhusu utendaji wa sekta ya Mifugo lakini kwa hili nililoliona leo nakiri wazi kuwa sasa yale maono ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan yanatimia na sasa nipo tayari kwenda kupiga magoti kwake ili bajeti tuongeze vituo vingine na bajeti ya Wizara iongezeke" Mhe. Dkt. Mpango.

Dkt. Mpango ameongeza kuwa hatua hiyo ya Wizara inatibu changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana wanaokadiriwa kuwa kati ya asilimia 60 hadi 70 ya idadi ya watu wote nchini.

"Kama ni mabadiliko ya kweli kwenye sekta ya Mifugo sasa ndo yanaanzia hapa kwa sababu haiwezekani sisi kama Taifa tunalojivunia kuwa la 3 kwa mifugo mingi lakini bado uuzaji wa nyama bora nje ya nchi upo chini na nimefurahi mmeamua kuanza kunenepesha ng'ombe wetu wa hapa hapa kwanza" Ameongeza Mhe. Dkt. Mpango.

Kwa Upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amemueleza Mhe. Dkt. Mpango kuwa takribani vijana 1600 wanahitimu ngazi mbalimbali za elimu kwa upande wa sekta ya Mifugo na kati yao 150 pekee ndo huingia kwenye mfumo rasmi wa ajira hivyo lengo la ubunifu huo ni kuwawezesha vijana wanaobaki kujiajiri kupitia shughuli hiyo ya unenepeshaji na uuzaji wa mifugo na mazao yake ndani na nje ya nchi.

"Mhe. Makamu wa Rais kinachofanyika hapa ni matokeo ya juhudi zenu wewe na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupa kazi ya kutafuta suluhu ya changamoto ya ajira kwa vijana na kutuwezesha pesa za kutekeleza mpango huu ambao kwa awamu hii umejumuisha vijana 240 kutoka pande mbalimbali za nchi yetu" Amesisitiza Mhe. Ulega.

Naye mmoja wa vijana hao Bi. Loyce Nyamoya mbali na kumshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuwawezesha kupata fursa hiyo aliwataka vijana wanawake kujitokeza kwa wingi kwenye awamu nyingine ili kuongeza idadi ya wawekezaji wanawake kwenye sekta ya Mifugo.

Mbali na vituo hivyo vilivyopo kwenye shamba la Mabuki, mpango huo pia unatekekelezwa Mkoani Tanga kwenye mashamba ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) na Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA) kampasi ya Buhuri na Mkoani Kagera kwenye Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA) kampasi ya Kikurula.

.