​PROF. MSOFFE AJA NA MIKAKATI MIPYA YA UENDESHAJI NARCO KIBIASHARA ZAIDI

Imewekwa: Thursday 01, July 2021

Meneja Mkuu wa Kampuni za Ranchi za Taifa (NARCO), Prof. Peter Msoffe ametaja mikakati itakayosaidia kampuni hiyo kuweza kujiendesha kibiashara Zaidi.

Prof. Msoffe ameibainisha mikakati hiyo leo (01.07.2021) baada ya kumalizika kwa kikao cha makabidhiano ya ofisi na aliyekuwa Kaimu Meneja Mkuu wa NARCO, Masele Shilagi kilichofanyika kwenye ofisi hizo jijini Dodoma.

Akizungumzia mikakati hiyo, Prof. Msoffe amesema kuwa serikali inataka kampuni hiyo iwe kitovu cha umahiri wa masuala yote yanayohusu ranchi. Katika kuhakikisha hilo linafanikiwa ni lazima kampuni ijipange katika uzalishaji wa nyama ya kutosha iliyo bora, uzalishaji wa mifugo iliyo bora, kutoa mafunzo kwa wataalam na wafugaji, kujiendesha kibiashara na kuweza kupeleka gawio serikalini.

Aidha, amesema ana matarajio makubwa kuwa hayo yataweza kutekelezeka kwa kuwa yeye ameikuta kampuni ikiwa inaendelea kuimarika hivyo kwa kushirikiana na viongozi na watendaji wa kampuni wataweza kutekeleza mikakati hiyo ambayo itawasaidia kuweza kutimiza azma ya serikali kwa kampuni hiyo.

Naye Masele Shilagi ambaye alikuwa ni Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ranchi za Taifa amesema kuwa kampuni imekuwa ikiendelea kuimarika kimapato ambapo iliweza kujiendesha bila kutumia ruzuku kutoka serikalini. Pia wameweza kusimamia mapato na matumizi ambapo kampuni imekuwa ikipata hati safi.

Lakini pia amesema kampuni imeweza kupima baadhi ya ranchi zake na kushughulikia migogoro iliyokuwepo ikiwemo ya uvamizi wa wananchi kwenye maeneo ya ranchi. Aidha, Masele amewashukuru viongozi na watumishi wa NARCO kwa ushirikiano waliompatia kipindi cha uongozi wake na kuwaomba waendelee kutoa ushirikiano kwa Meneja Mkuu mpya.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Uzalishaji na Masoko, Stephen Michael amesema kuwa viongozi na watendaji wanao wajibu wa kujipanga vizuri ili kuhakikisha malengo na matarajio ya serikali yanatimizwa. NARCO inazo fursa nyingi kwenye uzalishaji wa nyama bora, mifugo bora, malisho na utoaji wa elimu kwa wafugaji.

Michael amesema katika kuhakikisha fursa zinatumika na mapato yanaongezeka kama serikali ilivyopanga, ni lazima uongozi uone namna bora ya kushirikiana na sekta binafsi lengo likiwa ni kuongeza uzalishaji na kuongeza mapato.

.