PROF. MSOFFE AIKABIDHI RASMI NARCO

Imewekwa: Wednesday 01, November 2023

Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ranchi za Taifa nchini (NARCO) Prof. Peter Msoffe amekabidhi rasmi majukumu ya usimamizi wa kampuni hiyo kwa kaimu Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo Bw. Bwire Mujarubi leo Oktoba 23, 2023 jijini Dodoma.

Prof. Msoffe ambaye amehudumu nafasi yake kwa takribani miaka miwili na miezi mitatu amemshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Riziki Shemdoe,viongozi na watendaji wegine wa Wizara hiyo kwa Imani kubwa waliyompatia iliyomfanya atekeleze majukumu yake kwa mafanikio katika kipindi chote cha wadhifa wake.

“Yapo mambo ambayo tumefanikiwa wakati wa uongozi wangu ambayo ni pamoja na kuongeza rasilimali watu, kuongeza uzalishaji wa mifugo na malisho ikiwa ni pamoja na kupata vifaa vya kutengenezea malisho hayo lakini muhimu zaidi tumefanikiwa kuboresha mahusiano kati ya Taasisi yetu na nyingine hivyo ninaondoka leo nikiwa na furaha na naamini nimeitumia vizuri kwa kadri ya uwezo wangu” Ameongeza Prof. Msoffe.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa kampuni hiyo Bw. Bwire Mujarubi amemshukuru Prof. Msoffe kwa kuwaongoza vema na kuwapa ushirikiano mkubwa uliowawezesha kutekeleza shughuli zao kwa ufanisi ambapo ameahidi kutumia nafasi hiyo aliyopewa kuendeleza yote yaliyokuwa yaliyoanzishwa na mtangulizi wake.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Masoko na Uzalishaji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Stephen Michael ambaye alishuhudia makabidhiano hayo kwa niaba ya Wizara amempongeza Prof. Msoffe kwa kazi aliyoifanya wakati wote akihudumu nafasi yake huku akitoa rai kwa uongozi mpya kuendelea kutekeleza Maono na dira ya Wizara hiyo ya kuhakikisha ranchi hizo zinakuwa nyenzo ya mabadiliko katika sekta ya ufugaji nchini.

.