​PROF. GABRIEL AZITAKA TAASISI KUTUMIA MFUMO WA ULIPAJI SERIKALINI.

Imewekwa: Thursday 03, September 2020

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel amezitaka taasisi zilizo chini ya Sekta ya Mifugo kuhakikisha wanatumia Mfumo wa Ulipaji Serikalini (MUSE).

Prof. Gabriel aliyasema hayo Septemba 2, 2020 alipokuwa akizungumza na washiriki wa mafunzo ya Mfumo wa Ulipaji Serikalini yaliyofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi jijini Dodoma.

akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo, Prof. Gabriel aliwataka kuhakikisha wanautumia mfumo huo kwa kuwa utasaidia kuongeza makusanyo ya mapato, utarahisisha ulipaji wa fedha pamoja na kutunza kumbukumbu za matumizi ya fedha.

“Kwa kutumia mifumo ya TEHAMA sisi Wizara ya Mifugo kupitia minada tu tumeweza kuongoza ukusanyaji wa mapato mfano mmoja ya mnada uliopo kanda ya Ziwa tulikuwa tukikusanya sh. 720,000 kwa siku lakini baada ya matumizi ya mifumo ya TEHAMA tunakusanya 7,500,000 kwa siku,” alisema Prof. Gabriel.

Pia aliwasisitiza washiriki kuhakikisha fedha zote zinazokusanywa zinaingizwa kwenye mfumo kabla ya kutumika kwani kwa kutofanya hivyo watakuwa wamekiuka taratibu.

Vilevile ameipongeza Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuendelea kuwatumia wataalam wa ndani kubuni mifumo mbalimbali ya ukusanyaji mapato pamoja na udhibiti wa matumizi ya mapato hayo.

Naye Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA, Bw. Tazari Kibola amesema kuwa mafunzo hayo yatawawezesha washiriki kujua namna ya kutumia mfumo wa Ulipaji Serikalini (MUSE) utakaosaidia kuongeza ukusanyaji wa mapato na udhibiti wake katika taasisi zao.

Pia amesema kuwa baada ya mafunzo hayo watakwenda katika taasisi hizo kuona kama kuna mapungufu ya mahitaji yanayohitajika ili mfumo huo uanze kutumika.

Akimshukuru Katibu Mkuu kwa niaba ya washiriki wa mafunzo, Mhasibu Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Bw. Dennis Samangwa Ndabiriwe amesema kupitia mafunzo hayo na mfumo utakapoanza kutumika utawasaidia kuongeza mapato, hivyo watakwenda kuainisha mahitaji ya mfumo na kuhakikisha wanaanza kuutumia.

Mafunzo hayo yamewahusisha Wahasibu, Meneja wa Fedha, Wataalam wa Manunuzi, Maafisa TEHAMA na Maafisa Bajeti kutoka taasisi za Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA), Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Wakala wa Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Bodi ya Nyama, na Bodi ya Maziwa.

.