PROF. GABRIEL AAGIZA UZALISHAJI WA CHANJO YA UGONJWA WA MIGUU NA MIDOMO MWAKANI!

Imewekwa: Monday 19, April 2021

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel ameagiza upatikanaji wa chanjo ya mifugo ya ugonjwa wa miguu na midomo (FMD) ifikapo mwakani ili bidhaa zitokanazo na mifugo ziweze kuuzwa katika masoko ya kimataifa.

Prof. Gabriel ameyasema hayo jana (16.04.2021) jijini Dar es Salaam wakati akifungua kikao cha baraza la wafanyakazi la Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), ambapo amemuelekeza Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo Prof. Hezron Nonga kusimamia utekelezaji wa uanzishwaji wa chanjo hiyo ili kuwezesha viwanda vinavyozalisha nyama zitokanazo na mifugo hapa nchini kupata masoko ya bidhaa zao katika nchi mbalimbali.

Aidha ameitaka TVLA kuhakikisha changamoto ya homa ya nguruwe inatatuliwa kwa kupatikana kwa chanjo yake na kutokomeza kabisa ugonjwa huo hapa nchini na kuondoa dhana iliyojengeka kwa baadhi ya wananchi kuwa baadhi ya mifugo imekuwa ikibaguliwa katika upatikanaji wa huduma mbalimbali zikiwemo za chanjo.

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Hezron Nonga amesema mkakati uliopo ni kuhakikisha mwaka ujao zinazalishwa chanjo tatu za mifugo ikiwemo ya kichaa cha mbwa ili kufikia ukomo wa ugonjwa huo kwa kuwa lengo la dunia ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 ugonjwa huo unatokomezwa duniani.

Pia amesema chanjo zingine za ugonjwa wa sotoka ya mbuzi na kondoo tayari hatua zaidi zinaendelea kufanywa na TVLA ili kuhakikisha mwaka ujao chanjo hizo zinazalishwa hapa nchini pamoja na kuzalisha chanjo ya mapele ngozi.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dkt. Stella Bitanyi amesema wakala hiyo tayari imezalisha chanjo ya saba ya homa ya mapafu ya mbuzi kati ya chanjo 13 za kimkakati na tayari imethibtishwa na maabara ya chanjo za mifugo Afrika na imepata cheti cha ubora na uzalishaji wake umeshaanza.

Dkt. Bitanyi amesema TVLA inatategemea kuzindua chanjo hiyo kati ya Mwezi Mei na Juni mwaka huu ili itangazwe na wafugaji waanze kuitumia pamoja na kuweka mikakati ya uwezo wa kuzalisha zaidi chanjo dhidi ya homa ya mapafu ya ng’ombe kwa kuagiza mashine yenye uwezo mkubwa zaidi wa kuzalisha chanjo hiyo.

Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) ambayo ipo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi inafanya jitihada mbalimbali kuhakikisha inazalisha chanjo 13 za mifugo ambazo ni za kimkakati.

.