​PINDA AWATAKA WADAU WA MIFUGO NA UVUVI KUCHANGAMKIA FURSA

Imewekwa: Thursday 20, July 2023

Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Pinda amewataka wadau wa sekta za mifugo na uvuvi nchini kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta hizo ili kujikwamua kiuchumi.

Mhe. Pinda amezungumza hayo (12.07.2023) jijini Dodoma wakati wa mkutano wa wadau wa sekta za mifugo na uvuvi kuelekea mkutano mkuu wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Barani Afrika (AGRF) utakaofanyika hapa nchini kuanzia Septemba 4 hadi 8 mwaka huu.

Amesema sekta hizo zimekuwa zikitoa mchango mkubwa katika familia ikihusisha akina mama na vijana na kwamba zikitumika vizuri zinaweza kubadilisha kwa kiasi kikubwa maisha katika ngazi ya familia na kuwataka wadau wa sekta hizo kuangalia fursa zitakazotokana na mkutano huo utakaofanyika Mwezi Septemba ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan atakuwa mwenyeji wa mkutano huo.

Ameongeza kuwa amefurahishwa na programu maalum ya vituo atamizi ambapo Wizara ya Mifugo na Uvuvi inawajengea uwezo vijana katika kuwapatia mafunzo ya ufugaji bora na mitaji ili kuweza kujitegemea katika tasnia ya ufugaji.

Kwa upande wake mgeni rasmi katika mkutano huo Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) ambaye amehamasisha wadau kuendelea kujisajili kwa njia ya mfumo wa kieletroniki ili kushiriki katika mkutano wa AGRF amesema mkutano huo ni fursa kwa wadau wa sekta za mifugo na uvuvi hapa nchini kubadilishana uzoefu na kufanya biashara pamoja na wadau wa sekta hizo kutoka nchi zingine za Afrika.

Mhe. Ulega amesema mkutano wa leo uliohusisha wadau wa sekta za mifugo na uvuvi kutoka maeneo mbalimbali nchini unatakiwa kuwa na matokeo chanya kwa kuhakikisha muda uliotumika unakuwa na faida katika mkutano mkuu wa AGRF 2023 ili kukuza sekta hizo kwa kuongeza masoko hususan ya kuuza bidhaa nje ya nchi.

Ameongeza kuwa sekta za mifugo na uvuvi zimekuwa zikiendelea kuchangia katika pato la taifa hivyo jitihada zaidi zinahitajika ili mchango wa sekta hizo uwe imara zaidi na watu wengi kuingia katika sekta za mifugo na uvuvi.

Amesema mkutano wa AGRF 2023 utaleta muonekano tofauti wa namna ya kufanya biashara ya mifugo na uvuvi kwa njia bora zaidi na yenye tija ili kuleta tija na kwamba wafugaji wa Tanzania watakuwa na mengi ya kubadilishana na wenzano kutoka nchi zingine za Afrika.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe akizungumza kwenye mkutano huo amesema wadau wa sekta ya mifugo na uvuvi watapata fursa ya kujisajili katika mfumo maalum na kujipatia elimu ya kutumia fursa zitakazojitokeza katika mkutano wa AGRF 2023.

Prof. Shemdoe amesema mkutano huo unatoa fursa kwa wadau kupata elimu katika kupata fursa za namna wanavyoweza kujikita zaidi na kupata manufaa ya mkutano wa Mwezi Septemba mwaka huu.

Wadau wa sekta za mifugo na uvuvi kutoka maeneo mbalimbali nchini wamehudhuria mkutano uliowakutanisha wadao hao ili kujiandaa na mkutano mkuu ambapo takriban wageni elfu tatu wanatarajiwa kushiriki mkutano huo kutoka nchi mbalimbali barani Afrika.

.