NDAKI AWATAKA WATUMISHI KUJIEPUSHA NA VITENDO VYA RUSHWA

Imewekwa: Thursday 22, April 2021

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amewataka watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kujiepusha na vitendo vya rushwa huku akionya kuwa yeyote atakayebainika kuhusika na vitendo hivyo hatua stahiki zitachukuliwa dhidi yake.

Ndaki aliyasema hayo wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Mifugo na Uvuvi, sekta ya Mifugo uliofanyika jijini Dodoma Aprili 20, 2021.

Akizungumza na Wajumbe wa baraza hilo, Ndaki aliwataka watumishi hao kuzingatia uadilifu na uwajibikaji katika utekelezaji wa shughuli za serikali huku akisema siyo vyema kwa mtumishi wa umma kutajwatajwa kuhusika na matukio maovu yanayoharibu taswira ya serikali.

"Niwaombe watumishi wote mjiepusha na vitendo vinavyokwenda kinyume cha Sheria za nchi na taratibu za kazi, haipendezi kuona mtumishi wa umma anatajwatajwa kwenye kashfa za rushwa, hili siyo jambo jema hata kidogo, epukeni rushwa,”alisema Ndaki

Aliongeza kuwa watumishi ni muhimu wakaheshimiana na kuzingatia nidhamu ya kazi, wajiepushe na vitendo vya ubabe na kudharauliana huku akisema kuwa kila mtu katika kazi ana umuhimu wake.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza hilo, Prof. Elisante Ole Gabriel alimuahidi Waziri Ndaki kuwa wamepokea maelekezo yake na watahakikisha wanayasimamia vizuri ili kuongeza tija na ufanisi katika kazi.

Prof. Ole Gabriel aliongeza kuwa kupitia baraza hilo wataendelea kuboresha bajeti ya sekta ya mifugo ili waweze kuwanyanyua wafugaji waweze kufanya ufugaji wa kisasa na kuachana na ufugaji wa mazoea.

.