MNYETI AHAMASISHA ULAJI WA CHAKULA SHULENI

Imewekwa: Wednesday 01, November 2023

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti, amehamasisha ulaji wa chakula shuleni wakati akiongoza zoezi la ugawaji wa mayai na dagaa kwenye shule ya msingi Bitale maalum iliyopo mkoani Kigoma leo 14.10.2023.

Mhe. Mnyeti, ameongoza zoezi hilo la uhamasishaji wa ulaji wa vyakula vyenye protini ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya chakula duniani yanayofanyika kitaifa mwaka huu mkoani Kigoma kuanzia Oktoba 10 hadi 16.

"Suala la lishe ni kitendawili kwa jamii zote za kitanzania na bado kuna umuhimu wa kutoa elimu zaidi kwa jamii juu ya ulaji wa lishe bora". Alisema Mnyeti

Vilevile, Mnyeti amesema kwa hapa Bitale wizara imekuja kufanya utekelelezaji wa kile ambacho tunakihamasisha na maeneo mbalimbali ambapo Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekuwa kinara katika jambo hili na tayari alishaingia mkataba na wakuu wa Mkoa yote Nchini.

Ameongezea kwa kutoa wito kwa wakuu wa Mikoa yote kuzingatia maelekezo ya Mhe. Rais aliyoyatoa wakati anaingia mikataba na wakuu wa Mikoa yote Nchini.

Naye, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma Bw. Albert Msovela ameishukuru serikali kuleta maadhimisho ya siku ya chakula Duniani mkoani kigoma kwani kwao wameichukua kama fursa kwa kutambua umuhimu wa Lishe kwa watoto na kila Mwananchi wa mkoa huo.

Msovela amesema kwa Mkoa wa kigoma bado kuna changamoto kwenye suala zima la Lishe kwa watoto, pia amemshukuru Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuleta fedha kwa maana ya Elimu bila malipo, nao kama Mkoa ameahidi kuwa watahakikisha mtoto anapata chakula muda wote awapo shuleni ili Kuongeza ufaulu.

Kwa upande wake mhudumu wa afya wa kitongoji cha Bitale shuleni, Bi. Subira Omary, amesema jukumu lake kubwa ni kuhamasisha Lishe kwa watoto.

"Asubuhi mtoto anapoamka anapaswa kunyonyeshwa, kisha na kuandaliwa uji ambao una mahindi, dagaa, karanga,sukari,kisha analishwa mtoto". Amesema Bi. Subira

Bi.Subira amesema baadhi ya wanakijiji hawawapi watoto chakula chenye lishe kutokana na kuwa na kipato kidogo ambapo huwa wanawapa watoto ugali na maharage mlo mmoja tuu,

Pia, Mwanafunzi wa shule ya Bitale maalumu, Asha Ntahondi, ambaye alikuwa anatafsiri Lugha ya alama kwa wanafunzi wa shule hiyo, ambao wana ulemavu wa kusikia amesema ameshukuru serikali kwa kuwaletea mayai ili kuweza kupata vitamini na kuweza kuongeza akili darasani

.