MIFUGO YA TANZANIA YAHITAJIKA VIETNAM NA WAZIRI NDAKI AWAALIKA WAVIETNAM KUFUGA SAMAKI

Imewekwa: Wednesday 28, April 2021

Balozi wa Vietnam nchini Tanzania Mhe. Nguyen Nam Tien amesema atawasilisha serikalini vigezo vinavyopaswa kufuatwa na wafanyabishara wa hapa nchini ili waweze kusafirisha mifugo na nyama kwenda nchini Vietnam, kutokana na nchi hiyo kuwa na uhitaji mkubwa wa nyama.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amebainisha hayo leo (28.04.2021) ofisini kwake katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, mara baada ya kuwa na mazungumzo mafupi na balozi huyo aliyefika ofisini kwa Waziri Ndaki ili kuimarisha mahusiano baina ya Tanzania na Vietnam na kupeana uzoefu katika sekta za mifugo na uvuvi.

Mhe. Ndaki amesema Balozi Tien amesema nchi ya Vietnam ina uhitaji mkubwa wa nyama kwa kuwa wana ng’ombe wasiozidi Milioni Sita hivyo kutoa fursa kwa wafanyabiashara wa Tanzania kuchangamkia fursa hiyo endapo watakidhi vigezo vya kusafirisha mifugo na nyama nchini humo.

“Tunaweza kutumia fursa hii kusafirsha ng’ombe au nyama na kwamba wataleta orodha ya vitu vinavyohitajika ili kama nchi tuweze kupeleka ng’ombe au nyama.” Amesema Mhe. Ndaki

Aidha, Waziri Ndaki amewaomba wawekezaji kutoka Vietnam kuwekeza hapa nchini katika viwanda vya maziwa kwa kuwa maziwa yaliyopo bado ni mengi kulinganisha na viwanda vilivyopo, pamoja na kuwekeza katika viwanda vya kuchakata ngozi za mifugo kwa kuwa kiasi kikubwa cha ngozi kimekuwa kikiharibika.

Kuhusu Sekta ya Uvuvi, Waziri Ndaki amesema amemuomba Balozi wa Vietnam hapa nchini Mhe. Nguyen Nam Tien kuwakaribisha wawekezaji kutoka nchini humo ili kuja kuwekeza katika ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba na mabwawa kwa kuwa nchi hiyo inafanya vizuri katika sekta hiyo.

Amefafanua kuwa lengo la serikali ya Tanzania ni kuwekeza zaidi katika ufugaji wa samaki ili idadi ya samaki wanaopatikana kwa njia ya maji ya asili kwa maana ya kwenye Bahari ya Hindi, maziwa na mabwawa iweze pia kupatikana kwa njia ya ufugaji wa kutumia vizimba na mabwawa.

“Tumewaomba kupata utaalamu wao wa ufugaji samaki, lakini pia kama tunaweza kupata wawekezaji kutoka kwao, tuna fursa kubwa na kama wizara tunataka tupate samaki nusu wanaotoka kwenye maji ya asili na nusu wengine wapatikane kwa njia ya kufuga.” Amesema Mhe. Ndaki.

.