MIFUGO NA UVUVI YAFA KIUME MBELE YA HAZINA

Imewekwa: Wednesday 01, November 2023

Timu ya soka ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekubali kipigo cha magoli 3-1 kwenye mchezo wa fainali ya Michuano ya SHIMIWI iliyokuwa ikifanyika mkoani Iringa leo Oktoba 14, 2023.

Huku timu zote zikionesha kandanda safi, Hazina walikuwa wa kwanza kupata goli kupitia kwa mshambuliaji wao Juma Suleiman dakika ya 4 kipindi cha kwanza kufuatia makosa yaliyofanywa na walinzi wa timu ya wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Hata hivyo timu ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi waliendelea kucheza kwa utulivu mkubwa na kujiamini na kupelekea kusawazisha goli hilo kupitia kwa mshambuliaji wake Joseph Buhigwe aliyeunganisha moja kwa moja krosi safi iliyochongwa na winga wake William Valentino.

Timu hizo zilienda mapumziko zikiwa zimetoshana nguvu kwa goli 1-1 huku kila upande kupitia kwa walimu wao ukiangalia namna ya kupata magoli zaidi kipindi cha pili.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku timu zote zikishambuliana kwa zamu ambapo Hazina walifanikiwa kuandika bao la pili dakika ya 78 kupitia kwa winga wao Walid Kombo lililodumu mpaka mwisho wa mchezo huo kabla ya mchezaji huyo huyo kufunga goli la 3 na la ushindi dakika ya 93 ya mchezo huo.

Hata hivyo ilipotimu dakika ya 94 timu ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutokana na presha kubwa iliyokuwa ikielekeza langoni mwa timu ya Hazina ilifanikiwa kupata mkwaju wa penati ambao haukuweza kuzamishwa kimiani kupitia kwa golikipa wake Nkana hivyo kufanya matokeo kubaki 3-1 mpaka mwisho wa mchezo huo.

Baada ya kushuhudia namna wachezaji wake walivyopigana kufa na kupona kwenye mchezo huo Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe aliongeza dau kwenye ahadi yake ya awali kwa kila goli ambapo alitoa shilingi 1,000,0000 badala ya 500,000 aliyoahidi kwa kila goli hapo awali.

Kwa matokeo hayo timu ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi inakamilisha mashindano hayo ikiwa nafasi ya pili kwa upande wa soka huku ikishika nafasi ya 3 upande wa riadha umbali wa mita 100, 1500 na 3000, kurusha Tufe na mbio za baiskeli wanaume.

.