​MAKATIBU WAKUU WAKUTANA KUJADILI MAANDALIZI YA NANE NANE 2020

Imewekwa: Friday 24, July 2020

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Kusaya leo (24.07.2020) ameongoza kikao cha Makatibu Wakuu wa wizara za kisekta kujadili maandalizi ya Maonesho ya Kilimo Nane nane yatakayofanyika kitaifa mkoani Simiyu kuanzia tarehe 01 Agosti, 2020.

Katika kikao hicho, Bw. Kusaya alieleza kuwa ni matarajio ya wizara ya kilimo na zile za kisekta kuona maonesho ya Nane nane mwaka huu yanakuwa tofauti katika kuleta mapinduzi ya, ufugaji na uvuvi ili wananchi wapate kuongeza tija na ufanisi kukuza uchumi wa kaya na taifa.

Kikao hicho kimehusisha Makatibu Wakuu ambao ni Prof. Riziki Shemdoe (Viwanda na Biashara), Prof. Elisante Ole Gabriel (Mifugo), Mhandisi Anthony Sanga (Maji) na Dkt. Rashid Tamatamah (Uvuvi) na Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Miriam Mmbaga pamoja na kamati ya maandalizi.

“Tunapenda kuona maonesho ya Nane nane mwaka huu yanakuwa tofauti na yaliyopita katika kuwafanya wakulima, wafugaji na wavuvi wabadilike kutoka katika kilimo cha kujikimu kuwa kilimo, ufaguji na uvuvi wa kibiashara kupitia elimu na teknolojia bora watakayojifunza kutoka kwa wataalam “ alisema Kusaya

Kikao kimezishauri Wizara, taasisi na wadau wa maonesho ya mwaka huu kujikita katika kuwasaidia wakulima,wavuvi na wafugaji kuongeza tija katika shuguli zao ili baada ya maonesho maisha yao yawe bora zaidi kiuchumi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel alisema wakulima wanahitaji elimu ya kubadilisha mtizamo hivyo matumizi ya vyombo vya habari kufikisha elimu kwa wakulima, wafugaji na wavuvi ni muhimu sana kwenye maonesho haya.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Prof. Riziki Shemdoe alisema ni vema kamati ya uratibu ikaweka utaratibu wa kuwakutanisha wafanyabiashara za mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi pamoja na wakulima kwenye maonesho hayo hususan Simiyu.

“Tuandae maeneo kwa ajili wa wafanyabiashara na wakulima, wafugaji na wavuvi kufanyia mazungumzo ya kukuza upatikanaji wa masoko na kutumia fursa za biashara ikiwemo kuwekeza katika viwanda” alisisitiza Prof. Shemdoe.

Maonesho ya Kilimo Nane nane mwaka huu yana kauli mbiu isemayo “Kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Chagua Viongozi Bora 2020”.

.