MAFUNZO REJEA KWA MAAFISA UGANI YATAJWA KUTATUA CHANGAMATO ZA SEKTA YA MIFUGO

Imewekwa: Friday 23, December 2022

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imepongezwa kwa kutoa mafunzo rejea kwa maafisa ugani kote nchini ikiwa ni njia mojawapo ya mikakati ya kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya mifugo nchini.

Mkuu wa Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro Mhe. Juma Irando amebainisha hayo leo (19.12.2022) wakati akifungua mafunzo rejea ya siku mbili kwa maafisa ugani kutoka Kanda ya Kaskazini inayohusisha mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara ambapo amesema baadhi ya maafisa hao wanaohudhuria mafunzo wanatakiwa kuwashirikisha maafisa wengine pamoja na wafugaji juu ya mafunzo hayo ili sekta ya mifugo iwe na tija zaidi.

Mhe. Irando amesema sekta ya mifugo imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali hali inayosababisha baadhi ya wafugaji kutofuga kibiashara hivyo mafunzo rejea yanayotolewa na wizara hiyo yataleta matokeo chanya kwa maafisa ugani ambao wanategemewa kuwahudumia wafugaji.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Bw. David Lekei amesema wafugaji katika wilaya hiyo wameanza kubadilika na kufuga kibiashara kwa kuwashirikisha maafisa ugani ili kuwapatia mafunzo ya ufugaji wenye tija.

Bw. Lekei amesema wafugaji wa Wilaya ya Hai wameanza kutambua juu ya uchaguzi wa mbegu bora za mifugo pamoja na malisho ambayo yatakuwa na matokeo mazuri ya mazao yatokanayo na mifugo yao ikiwemo nyama na maziwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani (Ugani) kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi amesema lengo la mafunzo rejea kwa maafisa ugani nchini ambapo wizara imepanga kuwafikia maafisa hao 800 kuanzia ngazi ya kijiji, kata na halmashauri katika mwaka huu wa fedha ni kuwajengea uwezo katika utendaji wao wa kazi.

.