MAAFISA UGANI 1058 WAFIKIWA NA MAFUNZO REJEA 2024

Imewekwa: Sunday 31, March 2024

MAAFISA UGANI 1058 WAFIKIWA NA MAFUNZO REJEA 2024

◼️ Ni zaidi ya lengo la awali la kuwafikia Maafisa Ugani 1000.

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imehitimisha zoezi la Mafunzo Rejea kwa Maafisa Ugani 1058 waliokuwa katika kanda mbalimbali ikiwa ni juu lengo la awali la kuwafikia Maafisa Ugani 1000.

Akizungumza kwenye tukio la ufungaji wa Mafunzo hayo lililofanyika Machi 28, 2024 Babati mkoani Manyara Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu kutoka Wizarani hapo Dkt. Charles Mhina ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Riziki Shemdoe amewataka Maafisa Ugani hao kuhakikisha wanaenda kufanyia kazi kwa vitendo teknolojia zote walizofundishwa wakati wote wa Mafunzo.

“Lengo kubwa tulilolenga kama Wizara kwenye Mafunzo haya ni kuhakikisha Maafisa Ugani wetu wanapata uelewa kuhusu mabadiliko ya Teknolojia na falsafa za kada hii ya usimamizi wa sekta ya Mifugo” Amesema Dkt. Mhina.

Aidha Dkt, Mhina aliwasisitiza Maafisa Ugani hao kuhakikisha wanaielewa na kwenda kuifanyia kazi teknolojia ya Uhimilishaji ili kwenda kuboresha Mifugo iliyopo kwenye maeneo yao na kuongeza tija kwa wafugaji ili waweze kufuga kibiashara.

“Lengo mama la Wizara ni kuwabadilisha wafugaji wetu waanze kufuga kibiashara lakini hilo halitawezekana kama wana ng’ombe wanaozalisha lita 2 za maziwa kwa siku badala ya lita 20 mpaka 40 kwa ng’ombe wa kisasa na wa kutupeleka huko ni nyie” Ameongeza Dkt. Mhina.

Akizungumza kwa niaba ya Wakurugenzi wa mikoa ya kanda ya Kaskazini Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Babati Bi. Upendo Mangali ameipongeza Wizara kwa kuendesha mafunzo hayo huku akitoa rai kwa Taasisi nyingine za Serikali kuiga mfano huo ili kuongeza ujuzi zaidi kwa wataalam wake.

“Watumishi wakijengewa uwezo maana yake wanajenga Imani kwa wananchi hususan wafugaji kwamba watapata huduma bora na elimu haina mwisho kila siku mambo yanabadilika kutokana na mabadiliko ya teknolojia hivyo naamini nyie ni “TOT” mtaenda kufundisha wake waliopo kwenye maeneo yenu” Amesema Bi. Mangali.

Akizungumza kwa niaba ya Maafisa Ugani wenzie Mshauri wa Mifugo wa Mkoa wa Manyara Bw. Issa Mzava ameahidi kwenda kufanyia kazi yale yote waliyofundishwa kwenye kanda zote kwa kuzingatia kasi na weledi mkubwa.

Mafunzo Rejea hayo kwa Maafisa Ugani upande wa Sekta ya Mifugo yalifunguliwa rasmi Machi 18, 2024 Kibaha Mkoani Pwani ambapo yalifanyika kanda zote nchini kwa lengo la kuwafikia Maafisa Ugani 1000 nchi nzima.

.