MAAFISA MADUHULI WATAKIWA KUHAKIKISHA WANAZIBA MIANYA YA UPOTEVU WA MAPATO KATIKA MINADA

Imewekwa: Wednesday 01, December 2021

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amewataka Maafisa Maduhuli wa Serikali katika Minada ya Upili na ile ya Mpakani kuziba mianya inayosababisha upotevu wa mapato huku akiwataka kuongeza ufanisi katika ukusanya wa maduhuli hayo.

Waziri Ndaki alitoa maagizo hayo alipofanya kikao na Maafisa hao jijini Dodoma leo Novemba 10, 2021 ambapo alisema Maafisa hao wanatakiwa kuongeza nguvu ya ukusanyaji kwani kwa tathimini waliyoifanya ya makusanyo ya robo mwaka hayakuwa mazuri sana kwa kuwa yamefika wastani wa asilimia 50 wakati lengo ni kufika asilimia 100.

Aliongeza kwa kuwataka Maafisa hao kutotoa vibali kwa wafanyabiashara kinyume na utaratibu huku akitaka kila mfanyabiashara awe na leseni na kupewa kibali cha kusafirishia Mifugo ndani na nje ya nchi.

Pia, amewaagiza Maafisa hao kuhakikisha wanadhibiti utoroshaji wa Mifugo katika mipaka ya nchi kwa sababu kitendo hicho kinapunguza mapato ya nchi.

Aidha, alitumia nafasi hiyo kuwaonya wale Maafisa watakaoshindwa kufanya kazi hiyo ipasavyo kuwa hawatasita kuwatoa katika nafasi hizo ili kupisha wale watakaoweza kuifanya kazi hiyo vizuri.

Kuhusu Minada ya awali ambayo haijasajiliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Waziri Ndaki ameelekeza kuwa ni lazima isajiliwe, vinginevyo itafungwa mara moja kwa sababu wamegundua kuwa baadhi ya Minada hiyo inatumika kutoroshea mifugo kwenda nchi za jirani na kupoteza mapato ya Serikali.

.