ENEO LA MALISHO YA MIFUGO LILILOTENGWA NA SERIKALI KATIKA KIJIJI CHA MISUNA LAVAMIWA.

Imewekwa: Tuesday 23, April 2024

ENEO LA MALISHO YA MIFUGO LILILOTENGWA NA SERIKALI KATIKA KIJIJI CHA MISUNA LAVAMIWA.

Serikali kupitiaTume ya Taifa ya mpango wa matumizi ya Ardhi imetenga maeneo mbalimbali Nchini ikiwemo na maeneo ya malisho ya mifugo, Moja wapo ya maeneo hayo ni kijiji cha Misuna kilichopo wilaya ya Iramba Mkoani Singida ambapo wakazi wa kijiji hicho wamevamia eneo hilo liliotengwa na kufanya shughuli nyingine ikiwemo kulima Choroko.

Akiongea kwenye mkutano na baadhi ya wafugaji wa kijiji hicho Aprili 15,2024, Mkurugenzi msaidizi wa Idara ya Uendelezaji wa maeneo ya Malisho kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Gabriel Bura, amesema kijiji cha Misuna kimetengewa eneo la malisho ya Mifugo lenye ukubwa wa hekta 367.23 kwa ajili ya kulishia Mifugo ili kuondoa kabisa Migogoro ya wakulima na wafugaji.

Bw. Bura amesema wamefika kwenye kijiji hicho kwa lengo la kuhakiki maeneo yaliyotengwa na serikali na kufatilia uanzishaji wa mashamba darasa ya malisho katika maeneo hayo, lakini wakazi wa maeneo hayo wamebadili matumizi na kuyatumia kulima kitu ambacho ni kinyume na mpango wa serikali.

"hivyo kwa yeyote anayetumia eneo hilo kwa ajili ya matumizi mengine huyo atakuwa amefanya uharifu hivyo achukuliwe hatua". Amesema Bw. Bura.

Naye mmoja wa wafugaji wa kijiji cha Misuna, Bw. Juma Longoi, amesema eneo lililotengwa na serikali baadhi ya wanakijiji wamebadilisha matumizi ya eneo la malisho pasipo utaratibu na kusababisha wafugaji kukosa sehemu ya kulishia mifugo.

"Watu waliovamia eneo la malisho wapewe katazo kubwa na kuachia maeneo hayo ili sisi wafugaji tupate kulishia mifugo yetu" Amesema Bw. Juma.

Aidha, Mwenyekiti wa kijiji cha Misuna Bw. Ramadhani Kitiku amemaliza kwa kusema tabia ya kutumia maeneo pasipo na uhalali si nzuri na hivyo atafatilia kwa ukaribu na kuwaita walivamia na kuwataka kuachia mara moja eneo lililotengwa kwa ajili ya malisho na kuwakabidhi wafugaji.

.