Nifanyeje?
- Zipi sifa za kuorodheshwa kama msaidizi wa mtaalam wa mifugo? (Enlisted Paraprofessional Assistant)
- Zipi sifa za kujiandikisha kama mtaalam msaidizi wa mifugo? (Enrolled Paraprofessional).
- Daktari wa mifugo asiye mtanzania (Foreigner) anasajiliwa vipi na Baraza.
- Daktari wa mifugo asiye Mtanzania anaweza kusajiliwa na kufanyakazi hapa nchini? (Temporary and permanent registration)?
ELIMU KUHUSU PROGRAMU YA UTOAJI CHANJO DHIDI YA MAGONJWA YA WANYAMA YA KIPAUMBELE YAANZA KUTOLEWA
Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza kutoa elimu kuhusu program ya utoaji chanjo dhidi ya magonjwa ya wanyama ya kipaumbele ambayo inatarajiwa kuanza kwa lengo la kudhibiti magonjwa ya mifugo.
Hayo yamesemwa leo (01.09.2023) na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Mhina baada ya kumalizika kwa semina iliyoandaliwa na Wizara hiyo kuhusu program ya utoaji chanjo dhidi ya magonjwa ya wanyama ya kipaumbele kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo iliyofanyika Bungeni Jijini Dodoma.
Dkt. Mhina amesema malengo makubwa ya Wizara ni kuhakikisha mifugo haipotezi ubora au kufa kutokana na magonjwa wakati hayo yote yanaweza kuzuilika kupitia utoaji wa chanjo. Hivyo kupitia program hii ya uchanjaji tatizo la magonjwa kwa mifugo litakuwa limedhibitiwa kwa kiasi kikubwa.
“Katika semina hii tuliyoifanya kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo tumeweza kupokea maoni mengi yatakayosaidia utekelezaji wa program hii, kama namna ya upunguzaji wa gharama za chanjo na suala zima la utoaji wa elimu ya umuhimu wa uchanjaji mifugo kwa wafugaji na wadau wote wa sekta ya mifugo ili wote kwa ujumla wazingatie kalenda ya chanjo,” alisema
Dkt. Mhina amewahimiza wafugaji kuhakikisha wanachanja mifugo yao ili wawe na mifugo iliyokidhi vigezo vya kiafya vya kitaifa na kimataifa ambapo pia magonjwa kutoka kwenye mifugo kwenda kwa binadamu yatakuwa yamezuiliwa. Vilevile chanjo hizi zitasaidia kuongeza ubora wa mifugo na mazao yake na hivyo kukidhi viwango na mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi. Kuongezeka kwa ubora wa mifugo na mazao yake kutasaidia kuongeza kipato kwa wafugaji na mchango wa sekta ya mifugo kwenye pato la taifa.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Mariamu Ditopile Mzuzuri ameipongeza Wizara kwa kuandaa semina kuhusu Programu ya Utoaji Chanjo dhidi ya Magonjwa ya Wanyama ya Kipaumbele kwa wajumbe wa kamati hiyo kwani imesaidia kuwaongezeaa uelewa kuhusu shughuli zinazofanywa na sekta ya mifugo.
Bi. Mzuzuri amesema suala la chanjo ni muhimu sana kuzingatiwa na wafugaji, hivyo ni lazima kwanza elimu ya kutosha itolewa kwa wafugaji juu ya umuhimu wa chanjo na madhara ya kutochanja mifugo kwa kuzingatia kalenda iliyowekwa. Pia amesema kuwa zipo fursa nyingi katika mnyororo mzima wa biashara ya mifugo na mazao yake ambayo ikitumiwa vizuri itasaidia hata katika kutatua tatizo la upungufu dola lililopo hapa nchini na pia kuongeza mchango wa sekta kwenye pato la taifa.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Hester inayozalisha chanjo za mifugo, Bi. Tina Sokoine amesema kuwa wamekuwa na majadiliano mazuri na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ambapo wameweza kuelezea shughuli za uzalishaji wa chanjo zinazotengenezwa na Kampuni hiyo. Sokoine amesema kiwanda hicho kinazalisha chanjo 26 ikiwa ni pamoja na chanjo za magonjwa zaidi ya saba ya kipaumbele hapa nchini ambazo zote huuzwa ndani na nje ya nchi.