Nifanyeje?
- Zipi sifa za kuorodheshwa kama msaidizi wa mtaalam wa mifugo? (Enlisted Paraprofessional Assistant)
- Zipi sifa za kujiandikisha kama mtaalam msaidizi wa mifugo? (Enrolled Paraprofessional).
- Daktari wa mifugo asiye mtanzania (Foreigner) anasajiliwa vipi na Baraza.
- Daktari wa mifugo asiye Mtanzania anaweza kusajiliwa na kufanyakazi hapa nchini? (Temporary and permanent registration)?
CHINA YATOA VIFAA VYA UTAFITI KUKUZA SEKTA YA UVUVI NCHINI

Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China imetoa msaada wa vifaa vya utafiti wa maji baridi katika maziwa makuu kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wenye thamani ya dola za kimarekani 200,000 sawa na Shilingi za kitanzania Milioni 460 ili kukuza Sekta ya Uvuvi nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam (12.04.2023) mara baada ya kushuhudia mkataba wa makabidhiano ya vifaa hivyo vya maabara vitakavyopelekwa kwenye vituo vya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) ambapo vimetolewa na Taasisi ya NIGLAS kupitia Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amesema vifaa hivyo ni moja njia ya kuhakikisha Sekta ya Uvuvi inaleta matokeo chanya zaidi kwa kuhakikisha maziwa yaliyopo nchini yanakuwa na maji yaliyo bora kwa viumbe maji.
Awali, akifungua mafunzo ya namna ya kutumia vifaa hivyo kwa wataalamu wa utafiti TAFIRI pamoja na wataalamu kutoka nchi zinazoungana katika maziwa makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa, Prof. Shemdoe ameishukuru China kwa kuendelea kuiunga mkono Tanzania kwa kuhakikisha inatoa mafunzo yanayolenga kutoa ujuzi na wataalamu wa kutosha.
Ameongeza kuwa China imekuwa ikiisaidia Tanzania katika nyanja mbalimbali na kwamba mafunzo hayo yanayohusiana na usalama wa maji baridi yanalenga kubadilishana uzoefu wa namna ya kuhakikisha maji yanakuwa salama kwa viumbe maji wanaoishi katika maziwa hayo.
“Mafunzo ya kubadilishana uzoefu, watafiti wetu wa Tanzania watapata kutoka kwa wenzao wa China, ushirikiano huu ulisainiwa Mwaka 2008 kimsingi umesaidia katika mambo mbalimbali ya tafiti katika usalama wa maji na umesaidia wataalamu wetu 10 kupata shahada za uzamili na uzamivu.” amesema Prof. Shemdoe
Naye, Mwakilishi wa Balozi wa China nchini Tanzania, Bw. Suo Peng amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kujenga uhusiano mzuri kati ya Tanzania na China.
Bw. Peng amesema, mafunzo ya siku mbili yanayotolewa na China wataalamu wa Tanzania pamoja na nchi nyingine za maziwa makuu watafundishwa kuhusu matumizi ya vifaa vya kupima ubora wa maji baridi ambako samaki wanapatikana kwenye mazingira ambayo maji ni safi, ikolojia ya usalama wa maji na uvuvi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), Dkt. Ismael Kimirei amesema vifaa vya utafiti walivyopokea ni microscopes, vifaa vya kwenda uwandani kwenye maziwa na bahari, CTD kwa ajili ya kupima hewa ndani ya maji, kina cha maji, joto la maji, hali ya asidi na kuangalia vimelea kwenye maji ambapo awali TAFIRI hawakuwa nacho.
Dkt. Kimirei amefafanua kuwa, vifaa walivyokuwa navyo awali ni vya kuchuja maji yanayotumika maabara, ambapo teknolojia iliyopo ni kuchemsha maji na kugandisha mvuke ndio upate maji safi kwa ajili ya kutumika kwenye maabara, lakini mara nyingi yanakuwa bado na tindikali ndani yake.
“Pia teknolojia hii inatumia umeme mkubwa sana, ili kupata maji hayo kwa ajili ya kusafisha vifaa na kuvitumia kwenye maabara, kwa hiyo vifaa hivi vipya tulivyoletewa vitapunguza gharama ya kusafisha maji na kutupunguzia majukumu ya kuchemsha maji.” Amesema Dkt. Kimirei
Aidha amesema vifaa hivyo vitasaidia kupunguza gharama za kusafirisha sampuli nje ya nchi kwa ajili ya tafiti ambapo kwa siku kuna sampuli zaidi ya 1,000 zinasafirishwa kwa ajili ya uchambuzi.
“Sampuli za maji na sampuli za udongo mara nyingi tunazopeleka nje ni ‘genetics’ na madini tembo sehemu nyingine hapa nchini kufanya analysis ni dola 10 kwa ‘parameter’ 1 sasa sampuli 10 ni dola 100.” Amebainisha Dkt. Kimirei.