​CHATO KUWA NA KITUO KIKUBWA ZAIDI CHA UZALISHAJI VIUMBE MAJI TANZANIA

Imewekwa: Thursday 09, July 2020

Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia sekta ya Uvuvi imeikabidhi kampuni ya ukandarasi ya Serikali ya Corporation Sol eneo na mkataba wa Ujenzi wa Kituo kikubwa cha Ukuzaji wa Viumbe Maji ili kazi hiyo ianze mara moja.

Makabidhiano hayo yaliyofanyika jana katika kijiji cha Rubambangwe kilichopo wilaya ya Chato mkoani Geita na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah ambaye mbali na kubainisha kuwa mradi huo utakuwa ni mkubwa kuliko yote hapa nchini, pia alielezea maeneo kadhaa yatakayohusiana na mradi huo.

Dkt. Tamatamah alisema kuwa mradi huo utajumuisha ujenzi wa mabwawa yatakayokuwa na uwezo wa kutoa zaidi ya tani 10 za samaki kwa mwaka, jengo la vitotoleshi vya samaki ambalo litakuwa na uwezo wa kutoa vifaranga zaidi ya milioni mbili kwa mwaka, jengo dogo la kutengeneza chakula cha samaki na eneo la kuhifadhia samaki hao.

“Lakini pia litajengwa jengo la utawala ambalo ndani yake kutakuwa na ofisi, na ukumbi mdogo wa mikutano, jengo la darasa kwa ajili ya kutoa mafunzo ya wiki mbili mpaka tatu kwa wakuzaji waviumbe maji wanaohitaji kujifunza au kuongeza ujuzi, ujenzi wa bweni na ukumbi wa chakula”, alisema Dkt. Tamatamah.

Aliongezea kuwa mradi huo utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 3.8 mpaka kukamilika kwake na tayari wizara ilishalipa fidia ya shilingi milioni 42 kwa wakazi waliokuwa wakifanya shughuli zao za kiuchumi katika maeneo hayo yenye ukubwa wa zaidi ya ekari 28.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ukuzaji Viumbe Maji ambao ndio wasimamizi wakuu wa kituo hicho pindi kitakapoanza kufanya kazi, Dkt. Nazaeli Madala alisema kuwa kituo hicho kitakuwa ni ufumbuzi wa changamoto ya uchache wa samaki wanaopatikana kwenye vyanzo vya asili.

“Kituo hiki kitahudumia mikoa yote inayozunguka kanda ya ziwa na maeneo jirani na ukanda huu na tutawafundisha wafugaji wa samaki, maafisa ugani wa fani ya ufugaji wa samaki na pia kituo kitatumika kwa ajili ya mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi wanaosoma katika ngazi mbalimbali huko vyuoni”, aliongeza Dkt. Madala.

Madala alibainisha kuwa kituo hicho kitawasaidia kupata muongozo wa kujenga vituo vingine katika maeneo yanayozunguka Ziwa Tanganyika, Nyasa na maeneo ya Pwani lengo likiwa ni kuhakikisha viwanda vyote vya samaki vilivyopo nchini havikosi malighafi.

Naye Afisa Mtendaji wa kijiji cha Rubambangwe Bi. Restituta Majura alisema kuwa mradi huo utawanufaisha sana wakazi wa kijiji hicho kwani mbali na kutoa ajira kwa wananchi watakaoshiriki kwenye hatua ya ujenzi, pia wanatarajia kunufaika na uwepo wa barabara itakayoelekea eneo la mradi ambayo pia inaelekea kwenye zahanati ya kijiji inayoendelea kujengwa.

Kabla ya kuelekea kwenye eneo la ujenzi wa kituo hicho, Dkt. Tamatamah akiwa na timu yake ya wataalam kutoka wizarani, walifika ofisini kwa Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe. Charles Kabeho ambaye aliishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kupeleka mradi huo kwenye Wilaya yake na kuahidi kufuatilia kwa karibu hatua zote za ujenzi wa kituo hicho hadi kitakapokamilika mnamo mwezi Oktoba 2020.

.