Nifanyeje?
- Zipi sifa za kuorodheshwa kama msaidizi wa mtaalam wa mifugo? (Enlisted Paraprofessional Assistant)
- Zipi sifa za kujiandikisha kama mtaalam msaidizi wa mifugo? (Enrolled Paraprofessional).
- Daktari wa mifugo asiye mtanzania (Foreigner) anasajiliwa vipi na Baraza.
- Daktari wa mifugo asiye Mtanzania anaweza kusajiliwa na kufanyakazi hapa nchini? (Temporary and permanent registration)?
BODI YATAKIWA KUWA BUNIFU KUBORESHA HUDUMA ZA LITA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel ameitaka Bodi Mpya ya Ushauri ya Wakala ya Vyuo vya Mifugo (LITA) kuwa bunifu ili kuboresha huduma na kuleta tofauti katika shughuli zao na kufikia malengo yake.
Prof. Ole Gabriel aliyasema hayo alipokuwa akifungua kikao kazi cha kwanza cha Bodi mpya ya ushauri ya LITA kilichofanyika jijini Dar es Salaam Julai 25, 2020.
Akizungumza katika kikao hicho, Prof. Gabriel aliwahimiza wajumbe wa bodi hiyo kutumia vyema taaluma zao na kuwa wabunifu katika kuhakikisha LITA inaboresha huduma zake na kuleta mabadiliko chanya ya kiutendaji ya Wakala hiyo.
"Nawaomba bodi mfanye kazi yenu vizuri na mfanye maboresho kadri itakavyowezekana, shirikianeni kwa ukaribu na wadau wengine ili kusaidia kuboresha shughuli zenu," alisema Prof. Gabriel.
Sambamba na hilo, Prof. Gabriel ameitaka bodi hiyo kuhakikisha inasimamia vyema rasilimali fedha za taasisi hiyo huku akiwaeleza kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina wakati wote amekuwa mkali na watu ambao wamekuwa wanatumia vibaya rasilimali za umma.
Aliendelea kueleza kuwa LITA wanaweze kufanikiwa katika shughuli zao endapo wataweka mikakati ya kuboresha eneo la masoko na habari ambalo litasaidia kutangaza na kuhamasisha jamii kupitia vyombo vya habari kutumia huduma zinazotolewa na LITA na kwa njia hiyo wataongeza mapato.
"Hii ni taasisi ya biashara hivyo ni muhimu kuitangaza vya kutosha ili watu waijue LITA ni nini, ipo wapi na inafanya nini, kwa kufanya hivyo kutaivuta jamii kutumia huduma zenu," alifafanua Prof. Gabriel.
"Serikali inayoongozwa na Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imefanya kazi kubwa mpaka sasa tumeingia katika uchumi wa kati, hivyo LITA ni lazima muhakikishe mnaenda sambamba na kasi hii ya uchumi wa kati kwa kuboresha huduma zenu ikiwemo kubuni vyanzo vingine vya mapato," aliongeza Prof. Gabriel.
Akiongea mapema katika kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Wakala ya Vyuo vya Mifugo (LITA), Dkt. Pius Mwambene alisema kuwa mpaka sasa taasisi hiyo imepata mafanikio kadhaa ikiwemo kuongezeka kwa udahili wa wanafunzi kutoka 798 mwaka 2012/13 hadi kufikia 3642 mwaka 2019/2020 huku akisema kuwa wameshaongeza Kampasi nyingine mbili ambazo ni Mabuki, Mwanza na Kikulula, Kagera.
"Kuanzia Mwaka jana tumeanza kutoa gawio katika mfuko mkuu wa Serikali ambapo tulianza kutoa kiasi cha shilingi milioni 50 mwaka jana na mwaka huu tumetoa milioni 100,"alifafanua Dkt. Mwambene
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya LITA, Prof. Malongo Mlozi alisema kuwa kufuatia kauli hiyo ya Katibu Mkuu watahakikisha kuwa wataweka utaratibu kwa kushirikiana na Menejimenti kuangalia mapato na matumizi ya fedha kila miezi mitatu, huku akieleza kuwa kwa nafasi yao wataendelea kutoa ushauri juu ya matumizi bora ya rasilimali umma.
Kuhusu suala la ubunifu alisema kuwa wataweka mipango mizuri kuhakikisha taasisi hiyo kupitia Kampasi zake inajiendesha kibiashara ili kujiongezea kipato.