​BIL. 4.6 KUWANUFAISHA WAVUVI TANGA NA PEMBA.

Imewekwa: Friday 19, May 2023

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na nchi ya Ireland wameanza utekelezaji wa mradi wa "Bahari Mali" wenye thamani ya shilingi Bil.4.6 ambao utavinufaisha vikundi 19 vya wanawake na vijana waliopo mkoa wa Tanga na Pemba.

Akizungumza katika hafla fupi ya uzinduzi wa mradi huo Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo ni ishara tosha ya namna Serikali ya Rais Dkt. Samia na Dkt. Hussein Ally Mwinyi zilivyodhamiria kukuza uchumi wa pande zote mbili kupitia sekta ya Uvuvi

"Katika utekelezaji wa mradi huu, kila kikundi kitapewa mafunzo ya ujasiriamali bure kabisa na baada ya kumaliza mafunzo hayo kila kikundi kitawezeshwa mtaji wa shilingi milioni 32 hivyo ni lazima tukubaliane kuwa mama amedhamiria kubadilisha maisha ya watanzania kupitia fursa mbalimbali anazozipata kwa sababu sote tunakubaliana hakuna Serikali inaweza kukupa mtaji wa hela zote hizo bure kabisa" Ameongeza Mhe. Silinde.

Mhe. Silinde amebainisha kuwa lengo la mradi huo linaenda sambamba na malengo ya Serikali ambayo ni kuboresha uchumi wa wananchi hasa kupitia kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Waziri Kindamba amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo utaongeza utalii endelevu baina ya Tanga na Pemba na kukuza mazingira ya utawala bora ya mkoa huo wakati wote wa usimamizi wake.

"Lakini pia kwa kuzingatia kuwa utajiri wetu upo baharini, tutakuwa na jukumu muhimu la kukuza uchumi wa buluu kwa hapa mkoani kwetu kwa sababu kile kinachofanywa kule Zanzibar ni lazima na hapa Tanga kifanyike kwa utaratibu ule ule hivyo ninawahamasisha wananchi wa hapa tutumie fursa hii ipasavyo" Amesisitiza Mhe. Kindamba.

Kwa upande wake mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Uvuvi na Uchumi wa Buluu kutoka Zanzibar Bw. Omar Mohamed amesema kuwa uchumi wa nchi yao unategemea shughuli za uvuvi kwa zaidi ya asilimia 60 hivyo mradi huo ni chachu ya kuendeleza jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kukuza uchumi wa nchi hiyo.

Akielezea utekelezaji wake, Mratibu wa mradi huo Dkt. Elinas Monga amesema kuwa mradi huo utatekelezwa kwa kipindi cha miaka 3 (2022-2025) katika Wilaya za Mkinga na Pangani (Tanga) na Micheweni na Mkoani (Pemba).

Mbali na utoaji wa mafunzo na fedha kwa ajili ya ukuzaji viumbe maji bahari, mradi huo unalenga kutunza na kuhifadhi rasilimali za bahari na Pwani, kuboresha uelewa na maarifa kwa wadau wanaohusika na ulinzi wa rasilimali hizo kuendeleza huduma za kiikolojia kwenye maeneo ya Tanga na Pemba.

.