BIL. 3.1 KUTUMIKA KWENYE UKUZAJI VIUMBE MAJI RUVUMA, LINDI

Imewekwa: Sunday 05, May 2024

BIL. 3.1 KUTUMIKA KWENYE UKUZAJI VIUMBE MAJI RUVUMA, LINDI

◼️ Mhagama asisitiza fedha zake ni za moto

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu imeanza utekelezaji wa mradi wa kuendeleza Lishe na Ufugaji endelevu wa Viumbe maji kwa wakulima wadogo thamani ya shilingi Bil. 3.1 uliozinduliwa mkoani Ruvuma Aprili 4, 2024.Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu imeanza utekelezaji wa mradi wa kuendeleza Lishe na Ufugaji endelevu wa Viumbe maji kwa wakulima wadogo thamani ya shilingi Bil. 3.1 uliozinduliwa mkoani Ruvuma Aprili 4, 2024.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama amewataka watendaji wote watakaosimamia utekelezaji wa mradi huo kuwa waaminifu na kuhakikisha fedha zote zinatumika kwa malengo ya mradi yaliyokusudiwa.

“Mkoa wa Ruvuma licha ya kuongoza kwenye uzalishaji wa mazao ya chakula bado tuna changamoto kubwa ya udumavu hivyo tunatamani wananchi wa mkoa wa Ruvuma muendelee kuboresha afya zenu kupitia lishe ya viumbe maji watakaozalishwa kupitia mradi huu” Ameongeza Mhe. Mhagama.

Aidha Mhe. Mhagama amesisitiza kuwa uzinduzi wa mradi huo utachagiza maendeleo ya kiuchumi na lishe kwa Halmashauri zote zinazoutekeleza ambapo ametoa rai kwa Halmashauri nyingine nchini kutenga fedha za utekelezaji wa miradi ya ukuzaji viumbe maji kwenye maeneo yao.

Akielezea namna watakavyosimamia utekelezaji wa mradi huo, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti amesema kuwa Wizara yake itahakikisha wataalam wake wanatumia muda mwingi kwenye usimamizi wa mradi huo ili uwe shamba darasa kwenye maeneo mengine watakayoutekeleza.

“Mradi huu utakuwa na mchango katika kuiwezesha sekta ya Uvuvi kuweza kufikia malengo ya kimkakati ikiwemo mpango kabambe wa Uvuvi 2022/2023 na 2036/2037, mpango wa maendeleo ya miaka 5 wa mwaka 2021/2022-2025/2026 na malengo mengine ya kikanda na kimataifa ikiwa ni pamoja na kuongeza mchango wa sekta katika pato la Taifa kutoka asilimia 1.8 hadi asilimia 10 ifikapo mwaka 2036/2037” Amesema Mhe. Mnyeti.

Awali akielezea jinsi mradi huo utakavyotekelezwa, Naibu Katibu Mkuu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Bw. Anderson Mutatembwa amesema kuwa mradi huo utatekelezwa kwa miaka 2 katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea (Ruvuma) na Halmashauri za Wilaya za Ruangwa na Mtama (Lindi) na lengo lake kuu ni kimarisha mifumo jumuishi ya chakula ili kuboresha usalama wa chakula, Lishe na Ustahimilivu kwa ajili ya kuongeza biashara ya mazao ya Uvuvi na ufugaji viumbe maji.

Mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa programu ya kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) inayofadhiliwa na Shirika la kimataifa la kuendeleza Kilimo (IFAD) ambapo Tanzania inakuwa nchi ya 3 kuutekeleza ikiungana na nchi za Kenya na Msumbiji.

.