BARAZA LA WAFANYAKAZI SEKTA YA UVUVI LATAKIWA KUSIMAMIA USHIRIKISHWAJI

Imewekwa: Sunday 23, May 2021

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amelitaka Baraza la Wafanyakazi Sekta ya uvuvi kusimamia ushirikishwaji wa watumishi katika utendaji kazi wa kila siku ili kuondoa manung’uniko pamoja kusisitiza uadilifu na nidhamu kwa watumishi wa umma.

Mhe. Ndaki amebainisha hayo leo (10.05.2021) jijini Dodoma wakati akifungua baraza hilo na kusisitiza umuhimu wa watumishi kushirikishwa katika utendaji kazi wa kila siku ambapo amedai kwa kufanya hivyo manung’uniko yatapungua.

Ameongeza kuwa lazima kuwepo umuhimu wa ushirikishwaji wa watumishi katika ufanyaji kazi katika vitengo vyote, kwa kuwa ni jambo la msingi mahali pa kazi, hasa kwenye mambo yanayohusiana na idara, vitengo na taasisi za wizara.

“Rai yangu kwenu juu ya jambo hili tuendelee kushirikishana kwenye mambo muhimu na yanayotuhusu kama wafanyakazi kabla ya kufikia uamuzi ili tufikie uamuzi kwa pamoja, tukifanya hivyo itasaidia sana kwenye mambo mengi yanayohusu maslahi yetu na ustawi wetu mahali pa kazi.” Amesema Mhe. Ndaki

Aidha, amewataka viongozi wa baraza hilo kusimamia nidhamu pamoja na kuchukua hatua pindi yanapotokea mambo ya ukosefu wa nidhamu mahala pa kazi na kusimamia mkataba wa huduma bora kwa wafanyakazi ambao una mambo ya msingi kama kutochelewa kazini, kukosa uadilifu na mambo ya kutoa na kupokea rushwa.

“Niwaombe sana ndugu wajumbe masuala ya uadilifu, uaminifu na nidhamu kazini ni masuala ya msingi sana uzuri ni kwamba kuna sheria na taratibu na kanuni zinazotuongoza katika mambo haya, kwa hiyo tunapaswa kuziangalia na kuziheshimu ili kwamba tuweze kutoa huduma kwa wananchi wakati kwa kadri tunavyotegemewa.” Amefafanua mhe. Ndaki

Amewataka pia wafanyakazi hao kujadili kwa ukamilifu bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2020/21 na mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha Sekta ya Uvuvi 2021/22.

“Mtapitia taarifa ya utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2020/21 na mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha sekta ya uvuvi 2021/22, nitumie fursa hii kuwaomba kujadili kwa ukamilifu taarifa zote hizo mbili kwa uwazi kwa kina kisha mtoe maoni yenu.” Amesema.

Awali Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi Sekta ya Uvuvi ambaye pia ni Katibu Mkuu anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah, amesema kikao hicho kitakuwa na agenda za wajibu wa mwajiri, Chama cha wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) na wajumbe wa baraza mahali pa kazi pamoja na agenda kuhusu taarifa ya utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2020/21 na mpango wa bajeti kwa mwaka 2021/22.

Kikao cha leo cha baraza hilo Sekta ya Uvuvi ni cha kwanza ambapo katika kipindi cha mwaka 2018 hadi 2020 kulikuwa kuna jitihada mbalimbali za kukamilisha taratibu za kuwa na baraza ikiwemo kuandaa mkataba wa hali bora kwa wafanyakazi na kutiwa saini na TUGHE.

.